• HABARI MPYA

  Tuesday, June 04, 2019

  KAPOMBE ASTAAJABISHWA NA TAARIFA ZA KUUMIA MAZOEZINI STARS WAKATI HAJARIPOTI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  BEKI wa Simba SC, Shomari Kapombe amestaajabishwa na taarifa za kuumia mazoezini kwenye mazoezi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars jana Uwanja wa Taifa Dar es Salaam inayojiandaa na Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zikazofanyika baadaye mwezi huu nchini Misri.
  Kapombe ameposti kwenye ukurasa wake wa Instagram kwamba hata hajaripoti kwenye kambi ya Taifa Stars yupo nyumbani kwake anaendelea na programu ya mazoezi yake binafasi.
  “Ni jambo la kusikitisha na linaloumiza kwa kiasi kikubwa kwa taarifa hii inayoendelea kusambazwa na vyombo vya habari na watu mbalimbali kuwa nimeumia, nimejitonesha jeraha langu, hakika hizi habari si za kweli kabisa na hazina uhakika na ukweli wowote,” amesema Kapombe na kuongeza;
  “Katika siku niliyoumia ni leo, najiuliza nitaumiaje nikiwa nipo nyumbani na kambini sijaingia au kufanya mazoezi na timu ya Taifa??? Mimi niko mzima na ninafanya mazoezi yangu vizuri nafuata programu yangu niliyoachiwa na Mwalimu wa Viungo wa Simba,”. 

  Uzushi; Shomari Kapombe amesema yuko fiti nyumbani kwake bado hajaripoti kambini Taifa Stars

  Kapombe amesema kwamba yeye na familia yake wameumizwa na taarifa hiyo ni kubwa na nzito kwao, hivyo anaomba vyombo vya habari kutoa taarifa iliyokuwa sahihi na yenye ukweli wa asilimia 100. 
  “Wana Simba na Watanzania wote, wapenda soka napenda kuwaambia kuwa mimi niko sawa na hakuna ukweli wowote kuhusu mimi kuumia tena hizi taarifa sio sahihi kwa wote waliyotoa taarifa hizi au kusambaza. Mungu nipe uvumilivu na haya yatapita,” amesema Kapombe.
  Kapombe, anayecheza nafasi zote za ulinzi na kiungo ni miongoni mwa wachezaji 39 walioitwa kwenye kikosi cha awali cha Taifa Stars kilichoingia kambini juzi hoteli ya White Sands mjini Dar es Salaam kwa maandalizi ya awali ya AFCON kabla ya kikosi kwenda Alexandria Juni 7.
  Kapombe ameitwa Taifa Stars akitoka kuwa nje kwa zaidi ya miezi saba akiuguza majareha aliyoyapata mwezi Novemba mwaka jana nchini Afrika Kusini alipokuwa mazoezini pia na kikosi cha timu ya taifa kilichokuwa kikijiandaa na mchezo wa kufuzu AFCON dhidi ya Lesotho.
  Kocha Emmanuel Amunike aliamua kumjumuisha katika kikosi hicho cha awali kilichotangaza mwezi Mei mwaka huu, baada ya mchezaji huyo kupona majeraha yake na kuanza mazoezi tayari kwa kurudi dimbani licha ya klabu yake ya Simba kutomtumia katika mechi za mwisho za Ligi Kuu Tanzania Bara.
  Mapema leo Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo alisema Kapombe amejitonesha mazoezini Taifa Stars, lakini ataendelea kufuatilia programu ya mazoezi hadi hapo mwalimu atakapotaja kikosi cha mwisho.
  Taifa Stars itaondoka na wachezaji 32 kwenda kambini mjini Alexandria, Misri baada ya kuchujwa saba na kati ya hao ni 23 tu watashiriki AFCON.
  Wachezaji wengine wataendelea kubaki kambini kwa maandalizi ya michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
  Kikosi cha kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike kitaanza na mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji wa AFCON, Misri Juni 13, mwaka huu Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria.
  Baada ya hapo Taifa Stars itacheza mechi zake tatu za Kundi C mfululizo ikianza na Senegal Juni 23, Kenya Juni 27 na kumaliza na Algeria Julai 1 kuangalia matokeo yake kama yataipeleka hatua ya mtoano.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAPOMBE ASTAAJABISHWA NA TAARIFA ZA KUUMIA MAZOEZINI STARS WAKATI HAJARIPOTI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top