• HABARI MPYA

  Sunday, June 02, 2019

  HONGERA SIMBA SC, AZAM FC SASA JIPANGENI MICHUANO YA AFRIKA

  MSIMU wa michuano ya nyumbani Tanzania umekamilika jana kwa timu ya Azam FC kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Lipuli FC ya Iringa jioni ya leo Uwanja wa Ilulu mjini Lindi.
  Pongezi kwa mfungaji wa bao hilo pekee kwenye mchezo huo, mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa aliyefunga bao hilo dakika ya 64 baada ya kumzidi nguvu, beki wa Lipuli FC Ramadhani Haruna Shamte na kumuacha chini, kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Mohammed Yussuf.
  Kwa ushindi huo, Azam FC inarejea kwenye michuano ya Afrika na itashiriki Kombe la Shirikisho, huku mabingwa wa Ligi Kuu, Simba SC wakicheza Ligi ya Mabingwa. 

  Azam FC wanakuwa mabingwa wa nne wa michuano hiyo tangu irejeshwe mwaka 2016, baada ya Yanga SC, Simba SC mwaka 2017 na Mtibwa Sugar mwaka 2018.
  Mwaka 2016 Fainali ilifanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, 2017 Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma na 2018 mambo yalikuwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.   
  Kwa Azam FC hilo linakuwa taji la tatu msimu huu, baada ya awali kutwaa Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame na baadaye Kombe la Mapinduzi, ikiwa chini ya kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm aliyeondolewa mapema mwaka huu baada ya timu kupoteza mwelekeo.
  Timu imeshinda taji la Azam Sports Federation Cup ikiwa chini ya makocha wa muda, Meja Mstaafu Abdul Mingange na Iddi Nassor ‘Cheche’, walimu wa timu za vijana waliopewa kikosi cha kwanza baada ya kufukuzwa kwa Pluijm na Juma Mwambusi aliyekuwa Msaidizi wake.  
  Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa aliwakabidhi Kombe mabingwa wapya wa ASFC baada ya mchezo katika Uwanja uliopendezeshwa kwa mapambo ya wadhamini, Azam TV.
  Beki wa zamani wa Simba SC, Paul Ngalema wa Lipuli FC alichaguliwa Mchezaji Bora wa Mechi, kiungo mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Seif Abdallah Karihe akapewa tuzo ya Ufungaji Bora na beki wa klabu hiyo, Aggrey Morris akapewa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano.
  Katikati ya wiki, Simba SC ilikabidhiwa Kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya sare ya 0-0 na wenyeji, Mtibwa Sugar katika mchezo wa mwisho Mei 28 Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
  Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems imemaliza Ligi Kuu na pointi 93, zikiwa ni saba zaidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC waliomaliza na pointi 86 katika nafasi ya pili, wakati Azam FC imeshika nafasi ya tatu kwa pointi zake 75. 
  Hilo linkuwa taji la pili mfululizo la ubingwa wa Ligi Kuu kwa Simba SC na la 20 jumla kihistoria baada ya awali kulibeba katika miaka ya 1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990, 1994, 1995, 2001, 2003, 2004, 2007, 2010, 2012 na 2018.
  Watani wao, Yanga SC ndio mabingwa mara nyingi zaidi wa Ligi Kuu, mara 27 wakiwa wamebeba taji hilo miaka ya 1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992, 1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2008, 2009, 2011, 2013, 2015, 2016 na 2017.
  Timu nyingine zilizowahi kubeba taji hilo ni Cosmopolitan 1967, Mseto SC ya Morogoro 1975, Pan African 1982, Tukuyu Stars ya Mbeya 1986, Coastal Union ya Tanga 1988, Mtibwa Sugar mara mbili 1999 na 2000 na Azam FC 2014.
  Wakati Simba SC ikitwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya pili mfululizo, Stand United ya Shinyanga imeungana na African Lyon kuteremka daraja baada ya kufungwa 2-0 na JKT Tanzania. 
  Nazo Kagera Sugar ya Bukoba na Mwadui FC ya Shinyanga zitamenyana na timu za Daraja la Kwanza, Pamba SC na Geita Gold kuwania kubaki Ligi Kuu katika mechi za mchujo.
  Pongezi kwa Simba SC na Azam FC kwa mafanikio yao msimu huu na bila shaka kwa pamoja wanafahamu ushindi wa mataji hayo ni tiketi ya kuwania mataji mengine makubwa Afrika, Kombe la Shirikisho na Ligi ya Mabingwa.
  Msimu huu Tanzania iliwakilishwa na Simba katika Ligi ya Mabingwa na Mtibwa Sugar katika Kombe la Shirikisho, washindi wa mataji ya Ligi Kuu na ASFC msimu uliopita.
  Mabingwa wa ASFC, Mtibwa Sugar hawakufika mbali kwenye Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kutolewa raundi ya pili na KCCA ya Uganda, wakati mabingwa wa Ligi Kuu, Simba SC waliendelea kuwa timu bora kihistoria nchini kwenye michuano ya Afrika baada ya kufanikiwa kufika Robo Fainali.
  Kufika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa yalikuwa mafanikio tosha kwa klabu na taifa kwa ujumla, lakini ni kwenda Robo Fainali lilikuwa jambo la kujivunia zaidi.
  Wazi mafanikio ya Simba SC yalitokana na kuwa na kikosi imara chenye wachezaji wazuri wakiwemo wa kigeni na mwalimu bora pia – na bila shaka ili kurudia mafanikio yake hayo, klabu hiyo inajua inapaswa kujipanga vyema.
  Kadhalika kwa Azam FC inayomilikiwa na mfanyabiashara mkubwa, Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake ili kufanya vizuri kwenye michuano ya Afrika wanahitaji kuwa na kikosi imara na benchi zuri la Ufundi – bila kusahau maandalizi ya uhakika.
  Pongezi kwa washindi hao wa mataji ya nyumbani na wakumbuke kuwa hiyo ni tiketi ya kucheza michuano ya Afrika ambayo inahitaiji kujipanga vyema kabla kwa kujenga timu imara na maandalizi mazuri.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HONGERA SIMBA SC, AZAM FC SASA JIPANGENI MICHUANO YA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top