• HABARI MPYA

  Thursday, May 02, 2019

  TSHISHIMBI NA MAKAMBO WAFUNGA YANGA YAICHAPA TANZANIA PRISONS 2-1 UHURU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABAO ya wachezaji kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kiungo Papy Kabamba Tshishimbi na mshambuliaji Heritier Ebenezer Makambo leo yameipa Yanga SC ushindi wa 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.
  Kwa ushindi huo, Yanga SC wanafikisha pointi 80  baada ya kucheza mechi 34 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, sasa ikiwazidi point inane mabingwa watetezi, Simba SC ambao hata hivyo wana mechi sita mkononi, wakati Azam FC ni ya tatu kwa pointi zake 66 za mechi 33.
  Katika mchezo wa leo Yanga SC walipata bao lao la kwanza kupitia kwa Rasta Papy Kabamba Tshishimbi aliyemalizia kwa kichwa mpira wa adhabu wa kiungo mwenzake, mzawa Ibrahim Ajibu Migomba dakika ya 23.

  Mshambuliaji Heritier Makambo leo amefikisha mabao 16 katika Ligi Kuu, Yanga SC ikishinda 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons  


  Ikawachukua dakika tisa tu Tanzania Prisons kusawazisha bao hilo, mfungaji Ismail Kada aliyetumia makosa ya mabeki wa Yanga kushindwa kuokoa mpira wa kona wa Salum Kimenya kwa kumchambua vizuri kipa Ramadhani Kabwili dakika ya 32.
  Muda mfupi baada ya kuanza kipindi cha pili, kocha Mkongo wa Yanga SC, Mwinyi Zahera alimpumzisha kiungo Jaffar Mohammed aliyemuanzisha beki ya kushoto na kumuingiza mtu sahihi katika nafasi hiyo, Mwinyi Hajji Mngwali dakika ya 54.
  Na dakika ya 66 mshambuliaji Mkongo, Heritier Ebenezer akaifungia Yanga SC bao la pili kwa kichwa akimalizia krosi ya beki wa kulia, Paulo Godfrey.
  Yanga SC iliendelea kutengeneza nafasi za kufunga, huku Tanzania Prisons wakisaka bao la kusawazisha, lakini milango yote ikawa migumu kupokea mabao zaidi. 
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ramadhani Kabwili, Jaffar Mohammed/Mwinyi Mngwali dk54, Paul Godfrey, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Jaffar Mohammed, Feisal Salum, Mrisho Ngassa, Mohammed Issa ‘Banka’/Said Juma ‘Makapu’ dk81, Heritier Makambo, Papy Kabamba Tshishimbi na Ibrahim Ajibu/Deus Kaseke dk77. 
  Tanzania Prisons; Aaron Kalambo, Michael Mpesa, Leonsi Mutalemwa, Nurdin Chona, Vedastus Muhambi, Jumanne Nimkaza, Salum Kimenya/Lambert Sabiyanga dk73, Ezekia Mwashilindi/Ramadhani Ibata dk81, Adam Adam, Ismail Kada na Benjamin Asukile.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TSHISHIMBI NA MAKAMBO WAFUNGA YANGA YAICHAPA TANZANIA PRISONS 2-1 UHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top