• HABARI MPYA

    Sunday, May 05, 2019

    SIMBA SC YAIPIGA TANZANIA PRISONS 1-0, BADO MECHI MOJA KUITOA YANGA SC KILELENI

    Na Mwandishi Wetu, MBEYA
    MABINGWA watetezi, Simba SC wameendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Tanzania Prisons 1-0 jioni ya leo Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
    Shujaa wa Simba SC alikuwa ni mshambuliaji wake nyota wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi dakika ya 11 baada ya kuwazidi mbio mabeki wa TP kufuatia pasi ndefu ya kiungo Mghana, James Kotei na kumpiga chenga kipa Aaron Kalambo kisha kutumbukiza mpira nyavuni.
    Kwa ushindi huo, Simba SC inafikisha pointi 78 baada ya kucheza mechi 30, sasa ikizidiwa pointi mbili tu na vinara, Yanga SC ambao hata hivyo wamecheza mechi nne zaidi Ligi Kuu ikiwa ukingoni.


    Kwa ujumla Simba SC inayofundishwa na kocha Mbelgiji, Patrick Aussems ilitawala mchezo kipindi cha kwanza na kutengeneza nafasi nzuri za kufunga, isipokuwa tu safu ya ulinzi ya Tanzania Prisons na kipa waom, Kalambo walijitahidi kuzuia.
    Prisons inayofundishwa na kiungo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Mohammed ‘Adolph’ Rishard ilizinduka kipindi cha pili na kujaribu kusukuma mashambulizi langoni mwa Simba SC, lakini kumfunga kipa namba moja wa nchi, Aishi Manula lilikuwa jambno gumu kwao.
    Kwa kipigo cha leo, TP inabaki na pointi zake 42 baada ya kucheza mechi 34 ikiendelea kushika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ingawa inaizidi pointi tano tu Biashara United ya Mara inayoshika nafasi ya 19 kwenye Ligi ya timu 20.
    Ikumbukwe timu mbili zitashuka mwishoni wa msimu na mbili zitacheza mechi za kuwania kubaki kwenye Ligi Kuu dhidi ya timu za Daraja la Kwanza.      
    Kikosi cha Tanzania Prisons kilikuwa; Aaron Kalambo, Michael Mpesa, Leons Mutalemwa, Nurdin Chona, Vedastus Mwihambi, Jumanne Nimkaza, Salum Kimenya/Cleophas Mkandala dk70, Ezekia Mwashilindi, Adam Adam, Ramadhani Ibata na Ismail Kada.
    Simba SC; Aishi Manula, Zana Coulibaly/Nicholas Gyan dk88, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Yussuf Mlipili, Erasto Nyoni, James Kotei, Clatous Chama, Muzamil Yassin, Meddie Kagere, Emmanuel Okwi/Jonas Mkude dk65 na Haruna Niyonzima/Hassan Dilunga dk81.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAIPIGA TANZANIA PRISONS 1-0, BADO MECHI MOJA KUITOA YANGA SC KILELENI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top