• HABARI MPYA

    Friday, May 03, 2019

    SIMBA SC YAENDELEZA UBABE LIGI KUU, YAITANDIKA MBEYA CITY 2-1 SOKOINE

    Na Mwandishi Wetu, MBEYA
    MABINGWA watetezi, Simba SC wametoka nyuma na kushinda 2-1 dhidi ya wenyeji, Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya jioni ya leo.
    Kwa ushindi huo, Wekundu wa Msimbazi wanafikisha pointi 75 baada ya kucheza mechi 29, ingawa inabaki nafasi ya pili, nyuma ya watani wao wa jadi, Yanga SC wenye pointi 80 za mechi 34, wakati Azam FC yenye pointi 66 za mechi 33 ni ya tatu.
    Katika mchezo huo, Mbeya City walitangulia kwa bao la mshambuliaji wake hodari, Iddi Suleiman ‘Nado’ dakika ya 21 kwa shuti la nje kidogo ya boksi baada ya kuwatoka walinzi wa Simba SC, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Juuko Murshid.


    Simba SC ikapata pigo dakika ya 31 baada ya beki wake, Paul Bukaba Bundala kuumia na kushindwa kuendelesa na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na kiraka, Erasto Edward Nyoni.
    Kipindi cha pili kocha Mbelgiji wa Simba SC, Patrick Aussems alikianza kwa mabadiliko, akimtoa kiungo Mohammed ‘Mo’ Ibrahim na kumuingiza mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Arnold Okwi.
    Na dakika ya 67 kiungo Jonas Gerald Mkude akaunganisha kwa kichwa mpira wa beki Mghana, Nicholas Gyan kutoka kulia kuipatia Simba SC bao la kusawazisha akitumia makosa ya walinzi wa Mbeya City na kipa wao, Owen Chaima kutoka Malawi kuucheza kwa macho mpira.
    Na Simba SC ikapata bao lake la ushindi dakika ya 84 baada ya mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere kuuparaza kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na beki Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
    Bao hilo liliwachanganya wachezaji wa Mbeya City na kuwaacha Simba SC watawale zaidi mchezo na kukaribia kupata bao la tatu kama si kosakosa. 
    Kikosi cha Mbeya City kilikuwa; Owen Chaima, John Kabanda, Mpoki, Ibrahim Ndunguli, Erick Kyaruzi, Philipo Owden, Medson Mwakatundu/Kenneth Kunambi dk81, Hamidu Mohamed/Victor Hangaya dk78, Mohamed Samatta, Frank Ikobela na Iddi Suleiman ‘Nado’.
    Simba SC; Deogratias Munishi ‘Dida’, Nicholas Gyan, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Paul Bukaba/Erasto Nyoni dk31, Juuko Murshid/Yussuf Mlipili dk60, Said Ndemla, Hassan Dilunga, Jonas Mkude, Meddie Kagere, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Emmanuel Okwi dk46 na Rashid Juma.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAENDELEZA UBABE LIGI KUU, YAITANDIKA MBEYA CITY 2-1 SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top