• HABARI MPYA

  Saturday, May 04, 2019

  SAMATTA AFUNGA BAO LA PILI KRC GENK YAISHINDILIA ROYAL ANTWERP FC 4-0 UBELGIJI

  Na Mwandishi Wetu, Genk
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana amefunga bao la pili, timu yake KRC Genk ikiibuka na ushindi wa 4-0 dhidi ya Royal Antwerp FC kwenye mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
  Samatta alifunga bao lake dakika ya 55, baada ya kiungo wa kimataifa wa Ukraine, Ruslan Malinovskiy kufunga la kwanza kwa penalti dakika ya 25, kabla ya mshambuliaji Mjapan, Junya Ito kufunga la tatu dakika ya 57 na kiungo Mbelgiji, Bryan Heynen Heynen kufunga la nne kwa penalti pia dakika ya 90 na ushei.
  Ushindi huo unaifanya Genk ifikishe pointi 50 katika hatua ya pili ya Ligi ya Ubelgiji, maarufu kama Chama Championship Round na kuendelea kuongoza, ikifuatiwa na Club Brugge yenye pointi 41.
  Mbwana Samatta akikimbia kushangilia baada ya kuifungia KRC Genk bao la pili katika ushindi wa 4-0 dhidi ya Royal Antwerp 

  Mbwana Samatta akimtoka beki wa Royal Antwerp jana Uwanja wa Luminus Arena  

  Kwa Samatta jana amefunga bao lake la 23 la msimu na la tatu katika Championship Round akiwa anaendelea kuongoza kwenye mbio za ufungaji bora. 
  Kwa ujumla, Samatta mwenye umri wa miaka 26, jana ameifungia Genk bao la 62 katika mechi 153 za mashindano yote tangu amejiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Katika ligi ya Ubelgiji pekee amefunga mabao 47 katika mechi 120, kwenye Kombe la Ubelgiji amefunga mabao mawili katika mechi tisa na Europa League amefunga mabao 14 katika mechi 24.
  Kikosi cha KRC Genk jana kilikuwa; Vukovic, Maehle, Aidoo, Dewaest/Seigers dk89, Uronen, Berge, Heynen, Malinovskyi/Wouters dk67, Ito, Trossard na Samatta/Gano dk84.
  Royal Antwerp FC; Bolat, Juklerod, Rodrigues/Bolingi dk77, Baby/Owusu dk63, Arslanagic, Simao/Refaelov dk68, Govea, Van Damme, Haroun, Yatabare na Mbokani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA AFUNGA BAO LA PILI KRC GENK YAISHINDILIA ROYAL ANTWERP FC 4-0 UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top