• HABARI MPYA

    Thursday, May 02, 2019

    MZIBA, SUNDAY MANARA, MAKUMBI WAMUUNGA MKONO DK. MSOLLA UENYEKITI YANGA SC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    NYOTA wa zamani wa Yanga, Sunday Manara, Makumbi Juma, Abeid Mziba na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ juzi walikuwa kivutio katika kampeni za mgombea uenyekiti wa klabu ya Yanga, Dk. Mshindo Msolla.
    Mkutano huo ulifanyika Manzese, Dar es Salaam ambao uliandaliwa na matawi ya Yanga Kanda ya Kinondoni, ambapo baada ya Mwenyekiti wa Matawi ya Yanga Kanda ya Kinondoni, Shaaban Bakari kutamka uwepo wa nyota hao ukumbi uliripuka shangwe kutoka kwa wanachama hao.
     “Tunao Sunady Manara, Abeid Mziba, Mohammed Hussein, Shaaban Katwila, Makumbi Juma na Ramadhan Kampira hebu njooni hapa mbele,” alitamka Mwenyekiti huyo wakati akiwatambulisha wachezaji hao.

    Mgombea uenyekiti wa klabu ya Yanga, Dk. Mshindo Msolla anaungwa mkono na watu wengi

    Akizungumza katika mkutano huo, Sunday Manara alisema wachezaji wa zamani wana imani kubwa na Dk. Msolla na kwamba ni jukumu la wanachama wa Yanga kumpigia kura Jumapili katika Uchaguzi Mkuu wa klabu.
    Alisema amesikia sera zake na kwa namna alivyoiona Yanga ni wakati sahihi wa kupata viongozi wa aina ya Dk. Msolla na kueleza ni mtu sahihi kwa wakati huu kuiongoza Yanga.
    Kwa upande wake Mziba, alisema wanachama wa Yanga wasifanye makosa Jumapili wapige kura kwa kiongozi ambaye anaujua mpira vizuri.
     “Tumesikia sera za wagombea mbalimbali, naamini wapo wagombea wazuri wamejitokeza tuwaunge mkono, “ alisema Mziba.
    Akizungumza katika mkutano huo, Dk. Msolla alisema ana uzoefu wa miaka 40 katika maeneo mbalimbali ya mpira wa miguu hivyo wampe ridhaa aiongoze Yanga.
    Dk. Msolla ambaye kwa sasa anafanya kazi kampuni ya masuala ya mbolea ya OCP ambayo ni ya Morocco, alisema mambo muhimu atakayoyapa kipaumbele ni kujenga umoja ndani ya klabu, kuendeleza mchakato wa mabadiliko ya katiba katika mfumo wa uendeshaji wa klabu.
    Mambo mengine ni kuendeleza miradi iliyopo na kuanzisha mipya, kuweka misingi ya utawala bora na kuweka misingi ya klabu kuwa na timu bora.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MZIBA, SUNDAY MANARA, MAKUMBI WAMUUNGA MKONO DK. MSOLLA UENYEKITI YANGA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top