• HABARI MPYA

    Thursday, May 02, 2019

    MLEZI WA SERENGETI BOYS, REGINALD MENGI AFARIKI DUNIA USIKU WA KUAMKIA LEO DUBAI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    ALIYEKUWA Mlezi wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys na mpenzi mkubwa wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, mfanyabiashara Reginald Abraham Mengi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo huko Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).
    Hata hivyo, haijaelezwa, Mengi aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa makampuni ya IPP, wamiliki wa vituo vya Redio One, East Africa na Televisheni ya ITV na East Africa alikuwa Dubai kwa sababu zipi na chanzo cha kifo chake ni nini, ingawa imeahidiwa taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
    Taarifa za msiba huo zimetolewa katika kurasa rasmi za mitandao ya kijamii za vyombo vyake mbalimbali vya Habari mapema leo na zikafuatiwa na salamu za rambirambi kutoka kwa watu mbalimbali, akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
    Mfanyabiashara Reginald Abraham Mengi amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Dubai, UAE

    Katika uhai wake pamoja na kutambulika kama mfanyabiashara mkubwa, bilionea aliyekuwa na moyo wa kusaidia watu wasiojiweza hususan walemavu, lakini pia Mengi alikuwa mdau mkubwa wa michezo.
    Alianza kutambulika kama mdau wa michezo mwaka 1996 alipojitokeza kuisaidia Yanga wakati mgogoro mkubwa na kushauri klabu hiyo igeuzwe kampuni ili iweze kujitegemea kuliko kutegemea misaada ya Watanzania wenye asili ya Kiasia.
    Lakini mwisho wa siku wazo lake lilipuuzwa, naye akaamua kuachana nao tangu wakati huo ingawa kumekuwa na taarifa za kuendelea kusaidia kila alipofikiwa kuombwa.  
    Ni katika miaka hiyo pia Mengi aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa Stars akishirikiana na aliyekuwa mfadhili wa klabu ya Simba SC, Azim Dewji.
    Mara ya mwisho kujihusisha na masuala ya michezo ni miezi miwili tu iliyopita alipoteuliwa kuwa Mlezi wa Serengeti Boys iliyoshiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U17) mjini Dar es Salaam ambayo aliahidi kumpa kila mchezaji Sh. Milioni 20 kama wangetwaa taji hilo.
    Hata hivyo, Serengeti Boys haikufanya vyema kwenye mashindano hayo baada ya kufungwa mechi zote za Kundi A na kutolewa mapema.
    Mtunzi huyo wa kitabu cha I Can, I Must, I Will kilichozinduliwa na Rais Magufuli pia alikuwa anamiliki kampuni za madini za IPP Gold Ltd na Handeni Gold na kwa mujibu wa orodha ya matajiri wa Afrika iliyotolewa mwaka 2014 na jarida la Forbes la Marekani utajiri wake ulikuwa na thamani ya dola za Kimarekani Milioni 560 wakati huo.
    Mzee Mengi aliyezaliwa mwaka 1944 mkoani Kilimanjaro, amefariki dunia kiasi cha miezi sita tangu kufariki kwa mkewe wa kwanza, Mercy Anna Mengi, usiku wa Novemba 1, mwaka 2018  katika hospitali ya Mediclinic Morningside Afrika Kusini alipokuwa akipatiwa matibabu.
    Mbali na Mercy, mama wa watoto wake watatu, Regina, Mutie (marehemu pia) na Abdiel, mke mwingine wa Mengi ni mwanamitindo na Miss Tanzania wa mwaka 2000 aliyewahi pia kuwa mwanamuziki, ambaye amezaa naye watoto wawili pacha. Mungu ampumzishe kwa amani Mee Reginald Abrahamu Mengi. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MLEZI WA SERENGETI BOYS, REGINALD MENGI AFARIKI DUNIA USIKU WA KUAMKIA LEO DUBAI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top