• HABARI MPYA

  Friday, April 05, 2019

  TWIGA STARS YALAZIMISHWA SARE YA 2-2 NA DRC MECHI YA KUFUZU OLIMPIKI YA 2020

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TANZANIA imeanza vibaya mbio za kuwania tiketi ya Fainali za Soka za Wanawake Olimpiki 2020 mjini Tokyo, Japan baada ya kulazimishwa sare ya 2-2 na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) usiku huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kwa matokeo hayo, Tanzania italazimika kwenda kushinda ugenini ili kuingia Raundi ya Pili ya mchujo wa kuwania tiketi ya Olimpiki 2020 ambako itamenyana na Equatorial Guinea.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Vistoria Shangula aliyesaidiwa na Olivia Amukuu na Paulina Joel wote wa Namibia, hadi mapumziko DRC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Wachezaji wa Twiga Stars wakishangilia bao la kusawazisha katika sare ya 2-2 na DRC leo


  Mwanahamisi Omar 'Gaucho' akimtoka mchezaji wa DRC leo Uwanja wa Taifa

  Bao hilo lilifungwa na Marilene Yav dakika ya 10 kwa shuti la umbali wa mita zisizopungua 27 ambalo lilimpita kipa wa Twiga Stars Najiat Abbas kama amesimama.
  Twiga Stars ikapoteza nafasi nzuri ya kusawazisha bao hilo baada ya mkwaju wa penalti wa beki Fatuma Khatib ‘Foe’, mzazi mwenzake kiungo mshambuliaji wa timu ya taifa ya wanaume, Simon Happygod Msuva kupanguliwa na kipa wa DRC, Fideline Mudimbi dakika ya 27.
  Penalti hiyo ilitolewa baada ya Monica Kanyinda wa DRC kamuangusha Deonisia Daniel wa Twiga Stars kwenye boksi.
  Kipindi cha pili Twiga Stars walirejea vizuri kwa kasi ya kushambulia na dakika ya kwanza tu, Deonisia Daniel akafunga kwa kichwa akimalizia krosi ya Stumai Aabdallah.
  DRC wakapata bao la pili lililofungwa na Grace Balongo dakika ya 53 akimalizia krosi ya Flavine Musolo iliyompita kipa Najiat Abbas.
  Twiga Stars ikasawazisha bao hilo kupitia kwa Asha Rashid ‘Mwalala’ aliyemalizia kwa kichwa krosi ya Deonisia Daniel, nyota wa mchezo wa leo.
  Mechi ya marudiano itachezwa Uwanja wa Martyrs, zamani Kamanyola mjini Kinshasa Aprili 9 na mshindi wa jumla atakutana na Equatorial Guinea katika Raundi ya Pili kati ya tano za mchujo wa kufuzu Olimpiki ya Tokyo 2020.
  Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Najiat Abbas, Wema Richard/Zena Khamis dk67, Amina Ally, Fatuma Issa, Deonisia Daniel, Mwanahamisi Omar ‘Gaucho’, Stumai Abdallah, Fatuma Khatibu ‘Foe’, Asha Rashid ‘Mwalala’, Enekia Kasonga na Happiness Hezron.
  DRC; Fideline Mudimbi, Emalaude Muyenga, Naomie Siala, Natacha Bakonga, Monica Kunyinda, Rachele Moseka, Ruth Monique/Merveille Makiese dk83, Marilene Yav, Flavine Musolo/Dorice Yangu dk58, Horinela Salu na Exaucee Ndjoli/Grace Balongo dk46.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TWIGA STARS YALAZIMISHWA SARE YA 2-2 NA DRC MECHI YA KUFUZU OLIMPIKI YA 2020 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top