• HABARI MPYA

    Thursday, April 04, 2019

    TAMBWE AKOSA PENALTI YANGA SC YATOA SARE 1-1 NA NDANDA FC NANGWANDA SIJAONA

    Na Mwandishi Wetu, MTWARA
    MATUMAINI ya ubingwa yamezidi kufifia Yanga SC baada ya kulazimisha sare ya kufungana 1-1 na wenyeji, Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara.
    Sare hiyo inaiongezea pointi moja Yanga SC na kufikisha 68 baada ya kucheza mechi 29, sasa wakiizidi kwa pointi sita tu Azam FC wanaofuatia katika nafasi ya pili – lakini furaha zaidi ni kwa mabingwa watetezi, Simba walio nafasi ya tatu na pointi zao 57 za mechi 22 tu kwani upinzani unazidi kupungua kwenye mbio za taji. 
    Kwa Ndanda FC na yenyewe baada ya kujiongezea pointi moja katika mechi ya 30 inafikisha 37 na kupanda hadi nafasi ya 11 kutoka ya 15. 

    Katika mchezo wa leo, Vitalis Mayanga alianza kuifungia Ndanda FC dakika ya 19 akitumia makosa ya beki Kelvin Yondan kushindwa kuutuliza mpira mrefu ulioingizwa na Kiggi Makassy, akamlamba chenga kipa Mkongo Klaus Kindoki na kufunga kiulaini.
    Dakika ya 28 Mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe alipiga nje mkwaju wa penalti uliotolewa na refa Martin Saanya baada ya beki Baraka Gamba Majogoro kumuangusha Heritier Makambo.
    Yanga SC ilifanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 61 kupitia kwa kiungo Papy Kabamba Tshishimbi aliyefunga kwa kichwa akimalizia kros ya Yondan aliyepanda kusaidia mashambulizi.
    Yanga SC iliendelea kupeleka mashambulizi mfululizo langoni mwa Ndanda ambao waliendelea kushambulia kwa kushitukiza. 
    Na dakika ya 90 refa Saanya alilazimika kushauriana na msaidizi wake namba moja, Abdallah Uhako baada ya mchezaji wa Ndanda kuonekana ameunawa mpira kwenye boksi, lakini wakakubaliana kutotoa penalti.
    Baada ya mechi, makocha wote, Mkongo Mwinyi Zahera wa Yanga na Khalid Adams wa Ndanda FC walimlalamikia refa Saanya kwa maamuzi yake.  
    Kikosi cha Ndanda FC kilikuwa; Said Mohammed ‘Nduda’, Aziz Sibo, Yassin Salum, Augustino Msata, Abdallah Mfuko, Emmanuel Memba, Hassan Maulid, Baraka Majogoro/Salub Chubi dk79, Mohammed Mkopi, Vitalis Mayanga na Kiggi Makassy/Atupele Green dk55. 
    Yanga SC; Klaus Kindoki, Paulo Godfrey, Jaffar Mohammed/Raphael Daudi dk81, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondan, Feisal Salum, Mrisho Ngassa/Thabani Kamusoko dk89, Papy Kabamba Tshishimbi, Heritier Makambo, Amissi Tambwe/Deus Kaseke dk51 na Pius Buswita.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAMBWE AKOSA PENALTI YANGA SC YATOA SARE 1-1 NA NDANDA FC NANGWANDA SIJAONA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top