• HABARI MPYA

  Thursday, April 04, 2019

  SIMBA SC YAPOKEA PONGEZI NZITO KUELEKEA MCHEZO WAKE NA TP MAZEMBE KESHOKUTWA

  Na Mwandishi Wetu, DODOMA
  WAZIRI Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameipongeza Klabu ya Simba kwa mafanikio iliyoipatia nchi msimu huu wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika.
  Ametoa pongezi hizo kwa klabu hiyo ya Msimbazi alipowasilisha hotuba bungeni mjini Dodoma leo kuhusu mapitio na mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake na Ofisi ya Bunge kwa mwaka wa fedha 2019/20.
  Amesema kwa muda mrefu klabu za Tanzania zimekuwa hazifanyi vizuri katika medani ya michuano ya klabu barani Afrika.
  "Katika msimu wa 2018/19, Klabu ya Simba ya Dar es Salaam imeweza kututoa kimasomaso baada ya kufuzu hatua ya robo-fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika." Majaliwa amesema.

  "Kufanya vizuri kwa Klabu ya Simba kunaongeza uwezekano wa Tanzania kupatiwa nafasi nyingine mbili na kufanya jumla ya klabu nne vitakavyoshiriki mashindano hayo makubwa barani Afrika katika msimu ujao.
  "Ushindi wa Taifa Stars na Simba una manufaa makubwa kwa nchi yetu ikiwamo kuitangaza vyema nchi na kufungua fursa za ajira kwa vijana wetu hususan wanaojihusisha na soka.
  "Nitumie fursa hii kuwapongeza wachezaji, viongozi, benchi la ufundi na mashabiki wote wa Klabu ya Simba kwa mafanikio hayo makubwa. Tupo pamoja nanyi.
  "Napenda pia kutumia fursa hii kumpongeza mwanamasumbwi wa kitanzania Hassan Mwakinyo kwa kuendelea kuwa mfano bora kwenye tasnia hiyo ya masumbwi. 
  "Machi 23, mwaka huu, Mwakinyo aliendelea kung'ara katika anga za masumbwi na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania baada ya kumtwanga mpinzani wake Muargentina Sergio Gonzalez huko Nairobi.
  "Nitoe wito kwa vyama vya michezo kuendelea kuwalea vema wanamichezo hususan vijana ili waipaishe Tanzania kwenye medani mbalimbali za michezo ndani na nje. Huu ni wakati wa kila mtanzania kuthamini michezo na kutambua kuwa michezo ni ajira na michezo inalipa."
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAPOKEA PONGEZI NZITO KUELEKEA MCHEZO WAKE NA TP MAZEMBE KESHOKUTWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top