• HABARI MPYA

    Monday, April 08, 2019

    SIMBA SC YAANDAA UTARATIBU KUPELEKA MASHABIKI WAKE LUBUMBASHI MECHI NA MAZEMBE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Simba SC imeandaa utaratibu wa mashabiki wake kwenda mjini Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kuisapoti timu hiyo kwenye mchezo wa marudiano Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, TP Mazembe Jumamosi ijayo. 
    Taarifa ya Simba SC jana jioni imesema kwamba kila shabiki anayetaka kuifuata timu Lubumbashi atalazimika kulipa kiasi cha Sh. 200,000 gharama ya usafiri wa barabara kwenda kurudi, pamoja na visa dola za Kimarekani 50 (Sh. 116,000).
    Lakini kila shabiki atatakiwa kuhakikisha ameandaa fedha zake za malazi kiasi cha dola 20 hadi 25 kuendelea kwa siku moja kwenye hoteli, hiyo ni mbali ya gharama zake za chakula na nyingine muhimu.  
    “Mwisho wa kupokea uthibitisho wa safari hii ni Jumanne, Aprili 9, 2019 Saa 10:00 jioni. Kwa wanaohitaji wawasiliane nasi kwa namba +255 745 346 687,”imesema taarifa ya Simba SC.
    Ikumbukwe Simba SC juzi ililazimishwa sare ya 0-0 na TP Mazembe katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Kwa matokeo hayo, Simba SC watalazimika kwenda kushinda ugenini kwenye mchezo wa marudiano Aprili 13 Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, au kutoa sare ya mabao ili wafuzu kwa mabao ya ugenini.
    Simba SC ilicheza vizuri mno Jumamosi na kuihimili TP Mazembe, mabingwa mara nne wa Ligi ya Mabingwa Afrika kiasi cha kukaribia kabisa kuibuka na ushindi Uwanja wa Taifa.    
    Dakika ya 31 mshambuliaji Mnyarwanda wa Simba SC, Meddie Kagere alipiga tik-tak nzuri kuunganisha krosi ya beki wa kulia, Zana Coulibally kutoka Burkina Faso, lakini mpira ukagonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya kuondoshwa kwenye eneo la hatari.
    Nahodha, Bocco akaikosesha timu yake bao la wazi dakika ya 48 baada ya kupiga nje akiwa anatazamana na kipa Muivory Coast, Sylvain Gbohouo kufuatia pasi nzuri ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima.
    Bocco tena dakika ya 53 akapiga mpira ukambabatiza kipa na kutoka nje baada ya kupewa pasi nzuri na kiungo Mzambia, Clatous Chama.
    Bocco akakamilisha siku yake mbaya kwa kukosa penalti dakika ya 59 baada ya shuti lake kupaa juu ya lango kufuatia beki Muivory Coast, Koffi Christian kuunawa mpira uliopigwa na Kagere akiwa nje kidogo ya boksi kulia.
    Kwa Mazembe, wao walitengeneza nafasi mbili tu za kusema walikaribia kupata bao, zaidi ya hapo waliutawala tu mchezo.
    Kwanza dakika ya nne mshambuliaji wake, Mkongo Jackson Muleka alipoangushwa na kipa Aishi Manula kwenye eneo la hatari la Simba SC, lakini refa Mustapha Ghorbal kutoka Algeria akamuonyesha kadi ya njano akidhani alijiangusha – pale asingeanguka kama angepiga ingekuwa habari nyingine.
    Nafasi nyingine nzuri mno Mazembe walipata dakika ya 89, baada ya mtokea benchi Glody Likonza kupiga shuti lililogonga mwamba wa kulia na kutoka nje akiwa amebaki yeye na kipa, Aishi Salum Manula.
    Zaidi ya hapo refa Mustapha Ghorbal alimaliza mpira wakati Mazembe wanajiandaa kupiga kona kutoka upande wa kulia wa Uwanja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAANDAA UTARATIBU KUPELEKA MASHABIKI WAKE LUBUMBASHI MECHI NA MAZEMBE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top