• HABARI MPYA

  Tuesday, April 09, 2019

  SIMBA SC KUIFUATA TP MAZEMBE KWA NDEGE MAALUM YA KUKODI IJUMAA WATARUDI JUMAMOSI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Simba SC inataka kuondoka na ndege maalum ya kukodi Ijumaa kwenda mjini Lubumbashi, DRC kwenye mchezo wa marudiano Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, TP Mazembe Jumamosi ijayo na watageuza mara tu baada ya mchezo, kwa matokeo yoyote.
  Ndege hiyo pia itakuwa nafasi kwa mashabiki, ambao kila mmoja atatakiwa kulipia dola za Kimartekani 500 nje ya visa dola 100 na kujigharamia malazi.
  Mashabiki wengine watasafiri kwa basi kwa gharama ya Sh. 200,000 nje ya visa dola 50 na malazi kiasi cha dola 20 hadi 25 kuendelea kwa siku moja kwenye hoteli.  
  Tayari Simba SC imelalamikia mabadiliko ya ghafla ya waamuzi wa mchezo huo yaliyofanywa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa sababu zisizo na mashiko.

  Marefa wapya walioteuliwa kuchezesha mechi hiyo ni mpuliza filimbi Janny Sikazwe, mshika kibendera wa pili, Romeo Kasengele refa wa mezani, Audrick Nkole wote wa Zambia pamoja na mshika kibendera wa kwanza Berhe Tesfagiorgis O'michael wa Eritrea.
  Marefa wa awali ni Bamlak Tessema Weyesa aliyepangwa kupuliza kipyenga, mshika kibendera wa kwanza Temesgin Samuel Atango wote wa Ethiopia, Gilbert Cheruiyot mshika kibendera wa pili na refa wa zamani Peter Waweru wote wa Kenya.
  Simba SC watakuwa wageni wa TP Mazembe Jumamosi Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi wakihitaji ushindi au sare ya mabao kwenda Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kufuatia kulazimishwa sare ya 0-0 katika mchezo wa kwanza juzi Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Simba SC ilicheza vizuri mno Jumamosi na kuihimili TP Mazembe, mabingwa mara nne wa Ligi ya Mabingwa Afrika kiasi cha kukaribia kabisa kuibuka na ushindi Uwanja wa Taifa baada ya Nahodha wake, John Raphael Bocco kakosa penalti dakika ya 59 kwa shuti lake kupaa juu ya lango kufuatia beki Muivory Coast, Koffi Christian kuunawa mpira uliopigwa na Meddie Kagere.
  Wakati huo huo, Beki Muivory Coast wa Simba SC, Serge Wawa Pascal anaweza kuukosa mchezo wa marudiano, baada ya kuumia kwenye mechi ya kwanza dhidi ya TP Mazembe Jumamosi iliyopita na Meneja Patrick Rweyemamu amesema leo ndiyo alikwenda kwenye vipimo.
  Lakini pia, Wawa mwishoni mwa wiki nyumba yake ilivamiwa na vibaka waliomuibia fedha taslimu dola za Kimarekani 1,000, shilingi kadhaa na nguo na viatu pamoja na vitu vingine vya kubebeka.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC KUIFUATA TP MAZEMBE KWA NDEGE MAALUM YA KUKODI IJUMAA WATARUDI JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top