• HABARI MPYA

  Friday, April 05, 2019

  SERENGETI BOYS YATWAA UBINGWA WA MICHUANO YA FERWAFA U17 KIGALI 2019

  Na Mwandishi Wetu, KIGALI
  TANZANIA imetwaa ubingwa wa michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka la Rwanda (FERWAFA) baada ya sare ya mabao 3-3 na wenyeji, Nyigu Wadogo mjini Kigali jana.
  Katika mchezo wa jana, mabao ya Serengeti Boys yalifungwa na John Edmund mawili dakika za 28 na 49 na Edson Mshirakandi dakika ya 89, wakati ya Rwanda yamefungwa na Rutonesha Henson dakika ya 18, Nsanzimfura Keddy dakika ya 20 na Isingizwe Rodrigue dakika ya 94.
  Kwa sare hiyo, Serengeti Boys inamaliza na pointi nyingi zaidi, nne kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya Cameroon kwenye mchezo kwanza Aprili 1.
  Wachezaji wa Serengeti Boys wakifurajia na Kombe na Medali zao jana baada ya kukabidhiwa mjini Kigali

  Siku hiyo, mabao ya Serengeti Boys yalifungwa na Abraham Maurice dakika ya tisa na Arafat Swakali dakika ya 90, la Cameroon likifungwa na Yannick Noah dakika ya 52.
  Cameroon imefuatia kwa pointi zake tatu baada ya kuifunga Rwanda 3-1 Machi 29 kwenye mchezo wa kwanza na kwa matokeo hayo wenyeji wameshika mkia kwa kuambulia pointi moja. 
  Michuano hiyo ilikuwa matayarisho ya mwisho kwa Serengeti Boys kabla ya kuingia kwenye Fainali za Kombe ka Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, (AFCON U17) katikati ya mwezi ambazo wao ndiyo wenyeji. 
  AFCON U17 2019 inatarajiwa kuanza Aprili 14, Tanzania ikifungua dimba na Nigeria Saa 10:00 jioni siku ambayo pia Nigeria itamenyana na Angola Saa 1:00 usiku Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Serengeti Boys itateremka tena uwanjania Aprili 17 kumenyana na Uganda kuanzia Saa 1:00 usiku baada ya Nigeria na Angola kupepetana kuanzia Saa 10:00 jioni.
  Serengeti Boys itakamilisha mechi zake za Kundi A kwa kumenyana na Angola Aprili 20 Uwanja wa Taifa huku Nigeria ikimenyana na Uganda Uwanja wa Azam Complex, Chamazi mjini Dar es Salaam, mechi zote zikianzia Saa 10:00 jioni.
  Ikumbukwe Kundi B linaundwa na timu za Guinea, Cameroon, Morocco na Senegal ambao mechi zao zitachezwa Uwanja wa Azam Complex kuanzia Aprili 15. Bingwa mtetezi, Mali hakufuzu kushiriki fainali za mwaka huu.
  Timu nne zitakazoingia Nusu Fainali, zitajihakikishia tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia za Vijana nchini Brazil baadaye mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SERENGETI BOYS YATWAA UBINGWA WA MICHUANO YA FERWAFA U17 KIGALI 2019 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top