• HABARI MPYA

  Friday, April 05, 2019

  MKUTANO WA KUPITISHA KATIBA MPYA TASWA KUFANYIKA APRILI 12 UWANJA WA TAIFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Marekebisho ya Katiba ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) imekamilisha hatua zote muhimu kuhusu marekebisho ya katiba hiyo na sasa imeitisha mkutano wa wadau wote Aprili 12 mwaka huu kwa ajili ya kuijadili na kuipitisha rasimu hiyo.
  Katibu wa Kamati ya Katiba ambaye pia ni Katibu Mkuu TASWA, Amir Mhando amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba Mkutano huo unatarajiwa kufanyika ukumbi wa Uwanja wa Taifa mjini hapa na Kamati ya Katiba inaamini mkutano huo utakuwa na tija katika kuboresha rasimu hiyo ili taratibu zingine ziendelee ikiwa ni pamoja na kupanga tarehe ya uchaguzi wa chama hicho.
  Mhando amesema kwa kuwa Kamati imekamilisha jukumu ililopewa la kuandaa rasimu hiyo, hivyo kilichobaki ni ushirikiano kutoa kwa wadau ili kumaliza jambo hilo.

  Pamoja na mambo mengine, Mhando amesema rasimu hiyo imeandaliwa kwa kuangalia Katiba za vyama mbalimbali duniani vinavyohusiana na waandishi wa habari za michezo na pia kupitia muongozo kutoka Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS), ambacho TASWA ni mwanachama.
  Amesema pia Kamati imechambua Katiba ya sasa ya TASWA na kupokea maoni kutoka kwa waandishi wa habari za michezo kuhusu maeneo yenye upungufu kwa nia ya kuiboresha.
  "Maeneo mbalimbali yamefanyiwa kazi  katika rasimu hiyo baadhi yakiwa ni sifa ya mwanachama, wajibu wa mwanachama, muundo wa uongozi, sifa za viongozi na pia ukomo wa uongozi. Pia kuna mapendekezo katika rasimu hiyo ya kuanzishwa kamati mbalimbali kwa nia ya kuisaidia Kamati ya Utendaji," alisema Mhando.
  Kamati ya Katiba ya TASWA imeundwa kutokana na agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe aliyeitaka BMT isitishe uchaguzi wa TASWA uliokuwa umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka jana na badala yake BMT ikutane na viongozi wa TASWA pamoja na baadhi ya wanahabari wa michezo kuona namna ya kuifanyia marekebisho Katiba ya TASWA iendane na wakati.
  Kamati ya Katiba inayoongozwa na Mwenyeketi wa zamani wa TASWA, Boniface Wambura ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), viongozi wengine ni Katibu wa Kamati Amir Mhando ambaye pia ni Katibu Mkuu wa TASWA na mwanahabari, Gift Macha ambaye ni Katibu Msaidizi wa Kamati.
  Wajumbe ni Katibu Mkuu wa zamani wa TASWA, Abdul Mohammed, Mhazini wa zamani wa TASWA, Nasongelya Kilyinga na wanahabari Thabit Zacharia na Devotha Kihwelo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MKUTANO WA KUPITISHA KATIBA MPYA TASWA KUFANYIKA APRILI 12 UWANJA WA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top