• HABARI MPYA

  Friday, April 05, 2019

  MABADILIKO MAKUBWA MIAKA NANE TANGU SIMBA IKUTANE NA MAZEMBE

  Na Frederick Daudi, DAR ES SALAAM
  MACHI 20 na Aprili 3 mwaka 2011 ni siku ambazo zinapokumbukwa na wapenzi wa Simba, kwa mbali  kizunguzungu kinaanza kuwaandama hasa wanapoelekea mechi ya Jumamosi hii dhidi ya TP Mazembe.
  Penati aliyofunga Emmanuel Okwi ilikuwa ni kama goli la kufutia machozi tu kwani Mazembe walifunga magoli 3 hivyo Simba ikachapwa 3-1 pale Lubumbashi katika mechi ya kwanza.
  Licha ya kupoteza mechi ile, Simba ilikuwa na matumaini makubwa ya kusonga mbele endapo wangeshinda angalau magoli 2-0 kwenye mechi ya marudiano katika uwanja wa Taifa. Wiki 2 baadaye, Jumapili ya Aprili 3, matumaini ya wanamsimbazi yale yakayeyuka.
  Mpaka dakika 90 zinamalizika, Simba ilifungwa mabao 3-2, Shija Mkina na Mbwana Samatta wakiifungia Simba lakini hayakutosha kupindua matokeo ya magoli ya akina Given Singuluma.
  Hizi mechi mbili zilitosha kabisa kumfanya Mbwana Samatta aonekane wa kimataifa hasa katika mechi ya pili iliyochezwa Taifa. Hatimaye, yeye pamoja na Patrick Ochan wakasajiliwa na TP Mazembe.
  Mbwana Samatta alikuwa mchezaji chipukizi kwenye kikosi cha Simba SC ilipomenyana na TP Mazembe mwaka 2011

  Simba ilikata rufaa dhidi ya Janvier Bukungu. CAF ilikubali rufaa hiyo hivyo Simba ikapewa ushindi na kusonga mbele, ikacheza dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco.
  Ni miaka 8 sasa tangu Simba icheze mechi ya mwisho na wababe hao wa Congo. Mambo mengi yamebadilika kwa timu zote mbili. Wale akina Kidiaba na Stopila Sunzu hawapo tena.
  Kikosi cha sasa cha Simba kinaonekana kiko vizuri ukilinganisha na kile cha kina Juma Kaseja, Kevin Yondani, Jerry Santo na Musa Hassan Mgosi waliocheza na Mazembe. Kipindi kile kocha alikuwa Patrick Phiri, sasa hivi kocha ni Patrick Aussems. Mchezaji pekee wa Simba aliyecheza mechi zile na anatarajiwa kucheza mechi hii, Emmanuel Okwi. 
  Huu ndio wakati wa Simba kuwafunga Mazembe. Mwaka 2011 Simba ilifungwa nje ndani. Mwaka huu ni zamu ya Simba kuwaondoa.
  Ni ukweli usiopingika kwamba TP Mazembe ni timu iliyofanikiwa katika michuano ya Afrika kuliko Simba. Ni wazi kwamba TP Mazembe wana uzoefu na michuano hii kuliko Simba. Ni dhahiri kwamba kikosi cha TP Mazembe, uwekezaji na gharama zao ni za juu ukilinganisha na Wekundu hawa wa Msimbazi. Hayo nakubaliana nayo kabisa.
  Lakini linapokuja suala la mechi hizi za mtoano, atakayezichanga karata zake vizuri kwa muda wa dakika 180 ndiye anayepata matokeo chanya. Mbinu za kocha pamoja na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja ndio mara nyingi huamua matokeo.
  Ni mechi ambayo Simba hawapaswi kucheza vizuri, bali kushinda. Yaani bora wacheze mpira wa hovyo lakini waibuke na ushindi. Nidhamu ya uwanjani, matumizi mazuri ya muda na nafasi ni vitu pekee vitakavyoipa Simba nafasi ya kuwatoa Wakongomani hawa. Mashabiki wako tayari kuiunga mkono timu yao pendwa kama ilivyokawaida yao kuujaza uwanja ule.
  Watanzania, wakiongozwa na rais wa nchi wako nyuma yenu wakiwa na shauku kubwa ya kuwaona wawakilishi wao pekee kwenye michuano ya Afrika wakivunja rekodi nyingine mwaka huu. Simba ina nia, uwezo na kila sababu ya kusonga mbele. Yes we can.
  (Mwandishi wa makala hii, Frederick Daudi ni m3wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kitivo cha Uandishi wa Habari (SJMC) na anapatikana kwa simu namba +255 742 164 329 na barua pepe; defederico131@gmail.com)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MABADILIKO MAKUBWA MIAKA NANE TANGU SIMBA IKUTANE NA MAZEMBE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top