• HABARI MPYA

    Saturday, April 06, 2019

    BOCCO AKOSA PENALTI SIMBA SC YALAZIMISHWA SARE NA TP MAZEMBE 0-0 TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imelazimishwa sare ya 0-0 na Tout Puissant Mazembe katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika jioni ya leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Hata hivyo, Simba SC watajilaumu wenyewe kwa sare hiyo ya nyumbani, kwani walipoteza nafasi nzuri mno ya kuibuka na ushindi kipindi cha pili, kufuatia Nahodha wake, John Raphael Bocco kukosa penalti.
    Kwa matokeo hayo, Simba SC watalazimika kwenda kushinda ugenini kwenye mchezo wa marudiano Aprili 13 Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, au kutoa sare ya mabao ili wafuzu kwa mabao ya ugenini.

    Dalili mbaya kwa Simba zilianza mapema tu dakika ya tano baada ya beki wake tegemeo wa kati, Muivory Coast Serge Wawa Pascal kuumia wakati anajaribu kuokoa mpira uliomtoka Jackson Muleka wa TP Mazembe na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Mganda Juuko Murshid.
    Kabla ya hapo, dakika ya nne refa Mustapha Ghorbal alimuonyesha kadi ya njano mshambuliaji Mkongo wa Mazembe, Muleka kwa kujiangusha kwenye eneo la hatari la Simba SC alipokutana na kipa wa Simba, Aishi Manula. 
    Dakika ya 18 beki wa kushoto wa Simba SC, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alionyeshwa kadi ya njano kwa kumuangusha Abdoulaye Sissoko wa TP Mazembe nje kidogo ya boksi.
    Dakika ya 31 mshambuliaji Mnyarwanda wa Simba SC, Meddie Kagere alipiga tik-tak nzuri kuunganisha krosi ya beki wa kulia, Zana Coulibally kutoka Burkina Faso, lakini mpira ukagonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya kuondoshwa kwenye eneo la hatari.
    Baada ya dakika 45 ngumu za kipindi cha kwanza, SImba SC ikakianza vizuri kipindi cha pili na dakika ya tatu tu Nahodha, Bocco akaikosesha timu yake bao la wazi baada ya kupiga nje akiwa anatazamana na kipa Muivory Coast, Sylvain Gbohouo kufuatia pasi nzuri ya kiungo Mnyarwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima.
    Bocco tena dakika ya 53 akapiga mpira ukambabatiza kipa na kutoka nje baada ya kupewa pasi nzuri na kiungo Mzambia, Clatous Chama.
    Bocco akakamilisha siku yake mbaya kwa kukosa penalti dakika ya 59 baada ya shuti lake kupaa juu ya lango kufuatia beki Muivory Coast, Koffi Christian kuunawa mpira uliopigwa na Kagere akiwa  nje kidogo ya boksi kulia.
    Kiungo Jonas Mkude naye akaonyeshwa kadi ya njano dakika ya 63 kwa kumshika Michee Mika akiwa anaondona na mpira. Okwi naye akaonyeshwa kadi ya njano dakika ya 80 kwa kumvuta jezi Muleka akiwa anaingia kwenye boksi.  
    Mazembe wakapoteza nafasi nzuri mno dakika ya 89, baada ya Glody Likonza kupiga shuti lililogonga mwamba wa kulia na kutoka nje akiwa amebaki yeye na kipa, Aishi Salum Manula.
    Refa Mustapha Ghorbal akamaliza mpira wakati Mazembe wanajiandaa kupiga kona kutoka upande wa kulia wa Uwanja.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa: Aishi Manula, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Serga Wawa/Juuko Murshid dk7, Jonas Mkude, James Kotei, Haruna Niyonzima, Meddie Kagere, Clatous Chama/Emmanuel Okwi dk55 na John Bocco.
    TP Mazembe: Sylvain Gbohouo, Joseph Ochaya, Tressor Mputu/ Glody Likonza dk81, Chongo Kabaso, Kevin Mondeko, Koffi Christian, Jackson Muleka, Rainford Kalaba/ Meschak Elia dk57, Godet Masengo, Abdoulaye Sissoko/Nathan Sinkala dk64 na Michee Mika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BOCCO AKOSA PENALTI SIMBA SC YALAZIMISHWA SARE NA TP MAZEMBE 0-0 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top