• HABARI MPYA

  Wednesday, March 06, 2019

  MEDDIE KAGERE ACHAGULIWA MCHEZAJI BORA WA LIGI KUU YA BARA MWEZI FEBRUARI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa timu ya Simba, Meddie Kagere amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Februari wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2018/2019.
  Kagere raia wa Rwanda ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Salim Aiyee wa Mwadui na Salum Kimenya wa Prisons alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). 
  Kwa mwezi huo wa Februari, Simba ilicheza michezo mitano na kushinda yote, ambapo Kagere alitoa mchango mkubwa kwa timu yake kupata pointi 15 akifunga mabao matano na Simba kupanda kwa nafasi moja kutoka ya nne iliyokuwepo mwezi Januari katika msimamo wa ligi inayoshirikisha timu 20. 
  Meddie Kagere wa Simba SC amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu mwezi Februari 

  Kwa upande wa Aiyee alikuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya timu ya Mwadui kwa mwezi huo, ambapo timu yake ilicheza michezo mitano ikishinda mitatu na kupoteza miwili ikipata pointi tisa na kupanda katika msimamo kutoka nafasi ya 15 hadi ya tisa na mshambuliaji huyo akipachika wavuni mabao manne. 
  Mafanikio ya Prisons kwa mwezi Februari ikishinda michezo yote mitano iliyocheza na kupata pointi 15 ikipanda kutoka nafasi ya mwisho katika msimamo wa ligi hadi ya 14 yamemuingiza katika fainali ya tuzo hizo mchezaji Salum Kimenya kutokana na uwezo mkubwa aliouonesha na kuisaidia timu yake kupata mafanikio hayo ikiwa ni pamoja na kufunga mabao matatu. 
  Pia Kamati ya Tuzo imemchagua Kocha wa Prisons ya Mbeya, Mohammed Rishard kuwa Kocha Bora wa mwezi Februari akiwashinda Kocha Mkuu wa Simba,  Patrick Aussems na Kocha Mkuu wa Mwadui, Ally Bizimungu. 
  Rishard ameonesha mabadiliko makubwa kwa Prisons muda mfupi tu baada ya kukabidhiwa timu hiyo ambayo haikuwa ikifanya vizuri, lakini baada ya ujio wake aliiongoza Prisons kushinda michezo yote mitano iliyocheza na kupata pointi 15 ikipanda kutoka nafasi ya mwisho katika msimamo wa ligi hadi ya 14. 
  Aussems yeye aliiongoza timu yake katika michezo mitano iliyocheza na kushinda yote ikivuna pointi 15 na kupanda kwa nafasi moja kutoka ya nne hadi ya tatu, wakati Bizimungu aliiongoza Mwadui kushinda michezo mitatu na kupoteza miwili ikipata pointi tisa na kupanda kwa nafasi mbili kutoka ya 17 hadi ya 15. 
  TFF ina utaratibu wa kuwazadiwa wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka 2017/2018  tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kategori mbalimbali.
  Washindi (Mchezaji na Kocha) kila mmoja atapata kitita cha sh. 1,000,000 (milioni moja) na tuzo (trophy) kutoka kwa wadhamini Biko Sports pamoja na kisimbusi kutoka kwa watangazaji rasmi wa TPL kampuni ya Azam TV.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MEDDIE KAGERE ACHAGULIWA MCHEZAJI BORA WA LIGI KUU YA BARA MWEZI FEBRUARI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top