• HABARI MPYA

  Wednesday, March 06, 2019

  MCHEZAJI WA 12 ANAYETEGEMEWA KUIPA SERENGETI BOYS UBINGWA

  Na Frederick Daudi, DAR ES SALAAM
  MICHUANO ya mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17 (AFCON U 17) inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Aprili 14 mwaka huu. Jambo la kipekee ni kwamba Tanzania ndiyo itakuwa mwenyeji wa michuano hiyo.
  Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kushiriki michuano hiyo, baada ya mwaka 2017 kuishia katika hatua ya makundi nchini Equatorial Guinea.
  Serengeti Boys ile iliyokuwa chini ya kocha Bakari Shime (Mchawi Mweusi) ilitarajiwa kufika mbali japo kutinga nusu fainali ili hatimaye wapate tiketi ya kucheza kombe la dunia la vijana. Lakini utofauti wa magoli ya kufunga na kufungwa ulitunyima nafasi ile na kuwashuhudia Niger wakiingia nusu fainali.

  Hatimaye akina Ramadhan Kabwili, Nikson Kibabage, Yohana Nkomola na wengineo ikawabidi warudi nyumbani mapema japo kishujaa.
  Mwaka huu Serengeti iko kundi A na Uganda, Angola na Nigeria na itafungua dimba dhidi ya Nigeria. Mabingwa watetezi, Mali pamoja na Ghana iliyofika fainali mwaka 2017, zimeshindwa kufuzu mwaka huu.
  Mwaka huu tunachezea kwenye ardhi yetu. Uwepo wa mashabiki wetu ni jambo ambalo litawatia nguvu sana vijana hawa. Tunachopaswa kufanya ni kuwaunga mkono vijana hawa chini ya kocha Oscar Mirambo.
  Tatizo kubwa la mashabiki wa Tanzania na hata kwingineko duniani, ni kukata tamaa mapema hasa wanapoona mambo yanaenda kombo. Kibaya zaidi, zile kelele ambazo wangetakiwa kupiga ili kuwatia nguvu wachezaji zinaanza kusikika wakiwazomea, kuwalaumu na  kuwatukana wachezaji wao. 
  Enyi Watanzania wenzangu, mnapaswa kutambua kwamba hawa vijana ni wadogo hivyo kuwazomea na kuwalaumu kutawachanganya zaidi. Hayo mambo muwafanyie akina Bocco na Yondani ambao hawawezi kuyumbishwa na mashabiki. Wao wameshazoea lakini si madogo hawa.
  Serengeti boys hawajazoea kucheza mbele ya umati mkubwa wa watu. Wanatarajia kuuona umati unaowaunga mkono. Ikitokea kuna dogo amekosea halafu akasikia Watanzania kadhaa wanamzomea, atazidi kuchanganyikiwa zaidi na kujikuta kufanya makosa makubwa. Tusiwachanganye kisaikolojia.
  Kuchezwa kwa michuano hii kwenye ardhi hii ya Magufuli pia kunaweza kukawa ni kikwazo kwa vijana hawa kuhimili  presha kutoka kwa Watanzania elfu 50 au 60 watakaokuwa uwanjani siku hiyo. Lakini kama tunawashangilia na kuwapa nguvu, ubingwa ni halali yao.
  Ni kweli wataingia uwanjani vijana 11 tu kuiwakilisha nchi yetu. Lakini amin amin nakwambia, nafasi yangu na yako katika mafanikio ya vijana hawa ni kubwa sana kwani sisi ni mchezaji wa 12 ambaye japo havai jezi kuingia uwanjani, mchango wake ni mkubwa mno. Chonde chonde Mtanzania, jiandae kuwaunga mkono Serengeti boys na si kuwazomea.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MCHEZAJI WA 12 ANAYETEGEMEWA KUIPA SERENGETI BOYS UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top