• HABARI MPYA

  Sunday, February 10, 2019

  SIMBA WANATAKIWA KUPIGANA KIUME WAZIFUNGE AL AHLY NA VITA

  Na Frederick Daudi, DAR ES SALAAM
  USHINDI katika vita unachagizwa na mambo mengi. Licha ya kuwa na silaha madhubuti, wingi wa wanajeshi na uimara wenu dhidi ya wapinzani, bado mnaweza mkapigwa na watu wanyonge lakini wenye mbinu na mipango mujarabu.
  Hivyo ndivyo ilivyo hata kwenye soka. Utajiri wa timu, aina ya wachezaji waliopo na uwekezaji wake hauifanyi iwe na garantii ya kushinda kila mechi dhidi ya kila timu ndogo. Hii ndiyo maana timu tajiri na kubwa duniani kama Manchester united, Real Madrid na Barcelona kuna wakati zinafungwa na timu dhaifu zinazoburuza mkia.
  Siku ya Jumanne Februari 12, wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika, Simba SC watakuwa na kibarua kigumu dhidi ya mabingwa wa kihistoria wa Afrika, Al Ahly ya Misri kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam. 
  Mtanange huu unakuja siku chache baada ya wekundu hao wa Msimbazi kufungwa magoli 5 na AS Vita kabla ya kupigwa kipigo kama hicho na Al Ahly. Kwa hali hiyo, Simba ambao hawapewi nafasi kubwa ya kufanya vizuri kwenye kundi hili, wanazisaka pointi 3 kwa udi na uvumba.
  Simba kama zilivyo timu nyingi za Afrika, imekuwa ikibebwa sana na matumizi mazuri ya uwanja wa nyumbani. Pale kwa Mchina pamekuwa pachungu mno kwa kila mgeni anayekuja. Kama hujui hilo waulize, Mbabane Swallows Nkana FC, na JS Soura watakusimulia vizuri kabisa bila kupepesa macho kile kilichowakuta.
  Kwa siku za karibuni, kipigo cha mabao 3-2 alichokipata Simba kutoka kwa Mashujaa kwenye michuano ya FA na kile cha 2-1 kutoka kwa Bandari kwenye SportPesa, vimewafanya baadhi ya wadau kuibeza Simba kwamba anafungika Taifa kirahisi. Wanaona kwamba ni dhambi Simba kufungwa na timu ndogo kwenye uwanja wa nyumbani. Lakini je, wajua? Hii haiwazuii Simba kuwachapa Waarabu na Wakongomani hapa.
  Ni kweli Simba inaonekana timu dhaifu zaidi "underdog" kwenye kundi hili. Ni kweli kuna utofauti mkubwa wa uwekezaji baina ya Simba na hawa kina Vita na Al Ahly. Hakuna ubishi kwamba kikosi cha Simba kinazidiwa mbali sana na aina ya wachezaji wa hivi vilabu vingine. Suala la mafanikio na uzoefu kwenye michuano ya kimataifa halina ubishi kwamba Simba inazidiwa. 
  Tuseme nini basi? Je, Simba icheze kwa uoga kisa inazidiwa? La Hasha. Lazima Simba wapambane. Kufungwa goli 10 ndani ya mechi mbili hakukufanyi upoteze alama nyingi zaidi ya aliyefungwa magoli 2 ndani ya mechi mbili. Simba bado ina nafasi ya kuingia robo fainali.
  Mpaka sasa Mnyama ana alama 3 katika nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi 3. Bado mechi 3 za hatua hii ya makundi ambapo mbili kati ya hizo Simba itakuwa nyumbani. Simba inapaswa kukusanya pointi 6 katika mechi za nyumbani na pointi moja dhidi JS Soura ugenini. Kama watafanya hivyo, watakuwa wamejikusanyia jumla ya alama 10 ambazo ni dhahiri zitawawezesha kufuzu.
  Simba haitakiwi kulipiza kisasi eti waichape Al Ahly au Vita goli 5 uwanja wa Taifa. Hapana. Hii ni ngumu na itawafanya washindwe kuukwea huu mlima. Simba inachohitaji ni ushindi tu. Haijalishi ni ushindi wa aina gani, cha msingi ni pointi 3 basi. 
  Mashujaa na Bandari waliifunga Simba kwa Mchina lakini Al Ahly na AS Vita inabidi wakae. Ni mechi ngumu sana lakini amin amin nakwambia, Simba wanatakiwa kuwa na juhudi zenye maarifa ya kupata pointi 6 zilizobaki nyumbani.
  (Frederick Daudi ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika  Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) anayepatikana kwa namba +255 742164329 na barua pepe: defederico131@gmail.com)
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA WANATAKIWA KUPIGANA KIUME WAZIFUNGE AL AHLY NA VITA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top