• HABARI MPYA

    Saturday, February 09, 2019

    SAMATTA APIGA ZOTE MBILI GENK YAWAADHIBU STANDARD LIEGE 2-0 LIGI YA UBELIGJI

    Na Mwandishi Wetu, GENK
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta usiku wa jana ameifungia mabao yote klabu yake, KRC Genk ikiibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Standard Liege kwenye mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
    Nahodha huyo wa Taifa Stars, alifunga mabao yake dakika za 67 na 87 akimalizia kazi nzuri ya mlinzi Mdenmark, Joakim Maehle katika mchezo uliokuwa wa upinzani mkubwa.
    Kwa ushindi huo, Genk inafikisha pointi 57 katika mechi ya 25 ya msimu, ikiendelea kuongoza ligi hiyo maarufu kama Jupiter kwa pointi 12 zaidi ya Club Brugge na Antwerp ambazo hata hivyo zimecheza mechi 24. 
    Mbwana Samatta akishangilia kibabe usiku wa jana baada ya kuifungia mabao yote KRC Genk ikiibuka na ushindi wa 2-o dhidi ya Standard Liege
    Mbwana Samatta akimtoka beki wa Standard Liege jana Uwanja wa Luminus Arena

    Aidha, Genk sasa inawazidi kwa pointi 14 wapinzani wao wa jana,  Standard Liege wanaoshika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo kubwa zaidi Ubelgiji.   
    Kwa Samatta mwenye umri wa miaka 26, jana amefikisha jumla ya mabao 58 katika mechi 141 za mashindano yote alizoichezea KRC Genk tangu amejiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Kwenye Ligi ya Ubelgiji pekee amefunga mabao 43 katika mechi 109, wakati Europa League amefunga mabao 14 katika mechi 22 na katika Kombe la Ubelgiji amefunga mabao mawili katika mechi tisa.
    Kikosi cha KRC Genk kilikuwa; Vukovic, Maehle, Aidoo, Dewaest, De Norre, Heynen, Malinovskyi, Pozuelo/Fiolic dk92, Paintsil/Ndongala dk78, Trossard/Ingvartsen dk85 na Samatta.
    Standard Liege; Ochoa, Vanheusden, Cimirot/Bastien dk52, Carcela, Marin/Kosanovic dk81, Djenepo, Bokadi, Lestienne, Cavanda, Laifis na Mpoku.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA APIGA ZOTE MBILI GENK YAWAADHIBU STANDARD LIEGE 2-0 LIGI YA UBELIGJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top