• HABARI MPYA

    Friday, February 08, 2019

    MKUTANO WA WAANDISHI WOTE WA HABARI ZA MICHEZO KUFANYIKA FEBRUARI 17 TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MKUTANO wa waandishi wote wa habari za michezo kujadili Rasimu ya Kwanza ya Mapendekezo ya Marekebisho ya Katiba ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) sasa utafanyika Februari 17 mwaka huu ukumbi wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Katibu wa Kamati ya Katiba na Katibu Mkuu TASWA, Amir Mhando amesema kwamba awali mkutano huo ulikuwa ufanyike Februari 10, lakini kwa tarehe hiyo kumejitokeza changamoto ambazo zipo nje ya uwezo wa kamati, hivyo imeonekana ni busara usogezwe mbele kwa wiki moja.
    Ni imani ya Kamati ya Marekebisho ya Katiba kwamba wanahabari watajitokeza kwa wingi ili kwa pamoja tuweze kuipitia rasimu kwa pamoja kwa nia ya kujenga chama imara.
    Katibu wa Kamati ya Katiba na Katibu Mkuu TASWA, Amir Mhando amesema mkutano utafanyika Februari 10

    Kamati ya Marekebisho ya Katiba ya TASWA  imeandaa mapendekezo ya rasimu iliyoandaliwa kwa  kuangalia Katiba za vyama  mbalimbali duniani vinavyohusiana na waandishi wa habari za michezo na pia kupitia muongozo kutoka Chama cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari za Michezo (AIPS), ambacho TASWA ni mwanachama.
    Pia Kamati imechambua Katiba ya sasa ya TASWA na kupokea maoni kutoka kwa waandishi wa habari za michezo kuhusu maeneo yenye upungufu kwa nia ya kuiboresha.
    Maeneo mbalimbali yamefanyiwa kazi  katika rasimu hiyo baadhi yakiwa ni sifa za mwanachama, wajibu wa mwanachama, muundo wa uongozi, sifa za viongozi na pia ukomo wa uongozi. Pia kuna mapendekezo katika rasimu hiyo ya kuanzishwa kamati mbalimbali kwa nia ya kuisaidia Kamati ya Utendaji.
    Kamati ya Katiba ya TASWA imeundwa kutokana na agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe aliyeitaka BMT isitishe uchaguzi wa TASWA uliokuwa umepangwa kufanyika Novemba 25 mwaka jana na badala yake BMT ikutane na viongozi wa TASWA pamoja na baadhi ya wanahabari wa michezo kuona namna ya kuifanyia marekebisho Katiba ya TASWA iendane na wakati.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKUTANO WA WAANDISHI WOTE WA HABARI ZA MICHEZO KUFANYIKA FEBRUARI 17 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top