• HABARI MPYA

  Sunday, January 06, 2019

  YAHYA ZAYED ACHUKULIWA NA ISMAILIA YA MISRI KWA MKATABA WA MIAKA MITATU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Yahya Zayed anayechezea klabu ya Azam FC ya Dar es Salaam ameomdoka jana mjini Dar es Salaam kwenda Misiri kujiunga na klabu ya Ismailia ya huko.
  Zayed mwenye umri wa miaka 20 aliondoka kwa ndege ya shirika la Ethiopia moja kwa moja kwenda Cairo ambako imeelezwa akifika atasaini mkataba wa miaka mitatu.
  Na hiyo ni baada ya Ismailia, moja ya klabu kongwe nchini Misri kumalizana na Azam FC juu ya mchezaji ambaye alikuwa amebakiza mkataba wa miaka miwili.  
  Akisaini mkataba huo, Zayed atakuwa mchezaji wa pili wa Tanzania katika Ligi Kuu ya Misri, baada ya kiungo Himid Mao anayechezea Petrojet ambaye pia ni mchezaji wa zamani wa Azam FC.

  Yahya Zayed (katikati) amekwenda Misiri kujiunga na klabu ya Ismailia kwa mkataba wa miaka mitatu

  Himid, Nahodha Msaidizi wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars yupo katika msimu wake wa kwanza Misri baada ya kujiunga na Petrojet Juni mwaka jana akitokea Azam FC aliyoanza kuichezea tangu timu timu ya vijana. 
  Ikumbukwe, Agosti mwaka jana Zayed aliitwa kwa majaribio ya wiki mbili Bidvest Wits ya Afrika Kusini, lakini pamoja na kuvutiwa na kipaji chake na uwezo wake kwa ujumla, ikamruhusu kurejea Azam FC kukusanya uzoefu zaidi.
  Lakini wakati Bidvest Wits wanasubiri apate uzoefu zaidi, kijana anachukuliwa na vigogo wa Misri kwenda kuanza maisha mapya ya kisoka. 
  Zayed alikuwemo kwenye kikosi kilichoisaidia Azam FC kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame Agosti mwaka jana.
  Azam FC iliichapa Simba SC mabao 2-1 na kubeba Kombe la Kagame Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Julai 13, mwaka huu hiyo ikiwa ni mara ya pili kwao kutwaa taji hilo baada ya mwaka 2015.
  Mchezaji mwingine kwenye kikosi cha Azam FC kilichotwaa Kombe la Kagame, mshambuliaji pia, Shaaban Iddi Chilunda amechukuliwa kwa mkopo wa miaka miwili na Tenerife ya Daraja la Kwanza Hispania. 
  Chilunda amekwenda kuungana na mchezaji mwingine wa zamani wa Azam FC katika kikosi hicho cha Tenerife, Farid Mussa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YAHYA ZAYED ACHUKULIWA NA ISMAILIA YA MISRI KWA MKATABA WA MIAKA MITATU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top