• HABARI MPYA

    Tuesday, January 08, 2019

    SINGIDA UNITED, BANDARI KUFUNGUA DIMBA MICHUANO YA SPORTPESA CUP

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Singida United imepangwa kucheza mechi ya ufunguzi dhidi ya Kaimu bingwa wa Ligi Kuu ya Kenya, Bandari FC, katika michuano ya SportPesa Cup inayotarajiwa kutimua vumbi kwa msimu wa tatu mfululizo kuanzia Januari 22-27 katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.
    Ratiba hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu, iliwekwa hadharani na waandaaji wa michuano hiyo, kampuni ya michezo ya kubashiri ya SportPesa ambapo mabingwa mara 27 wa Tanzania Bara, klabu ya Yanga wataumana na mabingwa wa Ngao ya Jamii ya SportPesa, timu ya Kariobangi Sharks kutoka nchini Kenya majira ya saa 10:15 jioni katika mechi ya pili ya siku ya ufunguzi
    Mabingwa watetezi Gor Mahia wataumana uso kwa uso na Mbao FC kutoka jijini Mwanza siku ya Januari 23 majira ya saa nane kamili mchana huku mtanange wa mwisho kwa hatua ya robo fainali ukipigwa kati ya Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba SC watakaowavaa AFC Leopards majira ya saa 10:15 jioni.
    Mitanange ya nusu fainali itapigwa Januari 25 huku mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu ukipigwa January 27 majira ya saa 8:00 mchana ambayo ni siku ya mwisho ya mashindano.
    Nae Mkurugenzi wa Mashindano (TFF), Ndugu Salum Madadi amesema maandalizi yote ya shindano yamekamilika, huku akiwataka mashabiki wa soka nchini kujitokeza kwa wingi uwanjani kushuhudia mechi kali na za kusisimua.
    “Mashindano ya mwaka huu sio ya kukosa kwa kila mpenzi wa soka nchini huku tukiwa na Imani kuwa timu zetu zitafanya vizuri na kubakisha Kombe nyumbani.
    Bingwa wa mashindano atakutana uso kwa uso na timu ya Everton kutoka Ligi kuu ya Uingereza katika mechi ya kirafiki itakayopigwa nchi atakayotoka mshindi. Hii itakuwa ni mara ya pili kwa klabu ya Everton kuzuru Afrika Mashariki baada ya kufanya hivyo mwaka 2017 ambapo walicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Gor Mahia aliyekuwa bingwa kwa mwaka huo.
     “Ratiba hii inatudhihirishia kuwa tutakuwa na wiki ya msisimko wa soka jijini Dar es Salaam. Nipende kutoa rai kwa mashabiki na wapenzi wa soka kuhudhuria uwanjani kwa wingi kuunga mkono maendeleo ya soka la ukanda huu,” alisisitiza Tarimba Abbas, Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti SportPesa Tanzania.

    Mashindano ya SportPesa Cup yametajwa na wachambuzi wa soka kuwa jukwaa sahihi kwa wachezaji kupata fursa ya kuonekana kimataifa kama ilivyokuwa kwa mshambuliaji wa zamani wa Gor Mahia, Meddie Kagere and mlinzi Godfrey Walusimbi ambao wameweza kupata ofa kubwa za usajili baada ya kuonesha viwango maridhawa kwenye mashindano yaliyopita ya SportPesa Cup (zamani yakijulikana kama SportPesa Super Cup) yaliyofanyika Juni 2018 mjini Nakuru, Kenya.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SINGIDA UNITED, BANDARI KUFUNGUA DIMBA MICHUANO YA SPORTPESA CUP Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top