• HABARI MPYA

  Sunday, January 06, 2019

  SIMBA SC YAICHAPA KMKM 1-0 NA KUTINGA NUSU FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI

  Na Sada Salmin, ZANZIBAR
  BAO pekee la chipukizi Rashid Juma limeipa Simba SC ushindi wa 1-0 dhidi ya KMKM katika mchezo wa Kundi A Kombe la Mapinduzi usiku huu Uwanja wa Amaan, Zanzibar.  
  Kwa ushindi huo Simba SC inafikisha pointi sita baada ya kucheza mechi mbili na kujihakikishia kwenda Nusu Fainali wakiwa wamebakiza mechi moja dhidi ya Mlandege wenye pointi nne mbele ya KMKM wenye pointi moja, wakati Chipukizi haina pointi. 
  Juma aliyepandishwa kutoka kikosi cha timu ya vijana alifunga bao hilo dakika ya 83 akimalizia krosi iliyopigwa na kiungo Mzambia, Clatous Chama.

  Na Juma alifunga bao hilo zuri na muhimu dakika 10 tu tangu aingie kuchukua nafasi ya kiungo mwenza mzoefu, Shiza Kichuya. 
  Simba SC ilicheza vizuri kwa mara nyingine leo kama ilivyokuwa juzi ikiibugiza Chipukizi 4-1, lakini tu ilikosa bahati ya kuvuna mabao mengi.
  Simba SC ilipata pigo dakika ya 43 baada ya beki wake tegemeo, Erasto Edward Nyoni kuumia goti kufuatia kugongana na beki wa KMKM Hafidhi Mohammed na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Said Ndemla.
  Hiyo haikuzuia Simba SC kuendelea kutawala mchezo kwa pasi zake nzuri za hapa na pale wakishambulia na kuwakosakosa KMKM mabao kadhaa ya wazi.
  Kikosi cha Simba SC kinarejea Dar es Salaam kuendelea na maandalizi ya mwisho ya mchezo wa Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Saouara ya Algeria utakaofanyika Januari 12 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Na kikosi cha pili, Simba B kinakuja kuwapokea kaka zao katika mechi ya mwisho ya Kundi B na baadaye Nusu Fainali kabla ya fainali kama watafuzu Januari 13 kisiwani Pemba.  
  Kikosi cha KMKM kilikuwa; Nassor Abdallah, Hafidh Mohammed, Hassan Choum, Makame Hajji Mngwali, Richard Jovit, Brown Bruno Costa, Ibrahim khamis, Isihaka Said/Iliaya Suleiman dk58, Ventiraus John, Abrahman Chinga/Mudrik Muhibu dk59 na Mussa Ali Mbaru.
  Simba SC; Aishi Manula, Zana Coulibaly, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni/Said Ndemla dk43, Pascal Wawa, James Kotei, Mohammed ‘Mo’ Ibrahim/Hassan Dilunga dk62, Clatous Chama, John Bocco/Haruna Niyonzima dk55, Emmanuel Okwi na Shiza Kichuya/ Rashid Juma dk73.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAICHAPA KMKM 1-0 NA KUTINGA NUSU FAINALI KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top