• HABARI MPYA

  Sunday, January 06, 2019

  MWADUI FC YAITANDIKA KAGERA SUGAR 4-0, AFRICAN LYON YAIPIGA STAND UTD 2-0

  Na Mwandisi Wetu, SHINYANGA
  TIMU ya Mwadui FC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa mabao 4-0 Kagera Sugar ya Bukoba Uwanja wa Mwadui Complex, wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
  Shujaa wa ushindi wa Mwadui FC leo ni mshambuliaji wake, Salim Hamisi Aiyee aliyefunga mabao matatu peke yake dakika za 48, 67 na 83 wakati bao lingine la wenyeji limefungwa na Mwadui FC 4-0 Kagera Sugar Revocatus Richard dakika ya 45.
  Salim Aiyee anaungana na wachezaji wengine wawili tu waliopiga hat-trick awali katika Ligi Kuu msimu huu, ambao ni washambuliaji wa kigeni, Mrundi Alex Hakizimana Kitenge aliyekuwa Stand United na Mganda Emmanuel Okwi wa Simba SC.

  African Lyon ‘imeona mwezi’ baada ya kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Stand United

  Msimu uliopita wa Ligi Kuu jumla ya hat tric tano zilipigwa katika Ligi Kuu, moja Okwi, washambuliaji wazawa Shaaban Iddi Chilunda aliyekuwa Azam FC kabla ya kuhamia Tenerife ya Hispania na Marcel Kaheza aliyekuwa Maji Maji ya Songea kabla ya kuhamia Simba SC ambayo imemtoa kwa mkopo Gor Mahia ya Kenya.
  Hat trick nyingine mbili zote zilipigwa na mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa aliyekuwa Yanga SC kabla ya msimu huu kuibukia Azam FC.
  Kwa ushindi wa leo, Mwadui FC inafikisha pointi 24 baada ya kucheza mechi 20 na kupanda kutoka nafasi ya tisa, wakati Kagera Sugar inayobaki na pointi zake 24 baada ya kucheza mechi 18 inashuka kwa nafasi moja hadi ya 10. 
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, African Lyon ‘imeona mwezi’ baada ya kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Stand United Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam, mabao ya Jabir Azizi dakika ya 61 na Ramadhani Chombo ‘Redondo’ dakika ya 68, wakati Biashara United imelazimishwa sare ya 0-0 na Singida United Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara.
  African Lyon inafikisha pointi 16 na kupanda kwa nafasi moja hadi ya 18 kwenye Ligi Kuu ya timu 20, wakati Biashara inarudi nafasi ya 17 ikifikisha pointi 14 baada ya wote kucheza mechi 19 sasa.
  Ikumbukwe, Tanzania Prisons inaendelea kushika mkia katika Ligi Kuu kwa pointi zake 12 za mechi 19, japokuwa imebadilisha benchi la ufundi ikimuondoa kocha Bora wa Ligi Kuu msimu uliopita Mohammed Abdallah ‘Bares’ na kumchukua Mohammed ‘Adolph’ Rishard.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MWADUI FC YAITANDIKA KAGERA SUGAR 4-0, AFRICAN LYON YAIPIGA STAND UTD 2-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top