• HABARI MPYA

  Tuesday, January 08, 2019

  KADI ZA BENKI TU KUTUMIKA KWENYE UCHAGUZI WA YANGA JUMAPILI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  UCHAGUZI mdogo wa klabu ya Yanga utafanyika kwenye Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay mjini Jumapili ya Januari 13, mwaka huu huku wanachamaa wa kadi za benki tu zilizohakikiwa wakiruhusiwa kuingia.
  Taarifa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) leo imesema kwamba kadi zitakazotumika katika Uchaguzi ni kadi za Kitabu na kadi za Benki zilizohakikiwa.
  Taarifa hiyo iliyotolewa na Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Mario Ndimbo imesema kwamba Kampeni za kuelekea Uchaguzi huo zimefunguliwa rasmi leo.
  Akitangaza kufunguliwa kwa kampeni hizo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF Malangwe Mchungahela amewataka wagombea kufanya kampeni kwa amani bila kumchafua mwingine.

  Kama hamna kadi za benki msijisumbue kwenda kwenye uchaguzi Jumapili

  Mchungahela ameongeza kuwa kila mgombea anaruhusiwa kujinadi kokote ikiwemo katika tawi lolote la Young Africans.
  Naye Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Young Africans ambaye pia ni Msaidizi wa Kaimu Mwenyekiti Siza Lyimo amewataka Wanachama kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi huo utakaokuwa wa amani na utulivu.
  Amewataka Wanachama kupita mapema kwenye matawi yao kuhakiki kadi zao za Uwanachama ili kupunguza usumbufu siku ya Uchaguzi.
  Wagombea waliopitishwa katika nafasi ya Uenyekiti ni Dk. Jonas Benedict Tiboroha, Mbaraka Hussein Igangula na Erick Ninga, Umakamu Mwenyekiti ni Yono Kevela, Titus Eliakim Osoro na Salum Magege Chota..
  Wagombea wengine 16 wamepitishwa kuwania nafasi za Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ambao ni Hamad Ally Islam, Benjamin Jackson Mwakasonda, Sylvestre Haule, Salim Seif, Shafil Amri, Said Kambi, Dominick Francis, Seko Jihadhari, Ally Omar Msigwa, Arafat Ally Hajji, Frank Kalokola, Ramadhani Said, Leonard Marango, Bernard Faustin Mabula, Christopher Kashiririka na Athanas Peter Kazige.
  Uchaguzi wa Januari 13 mjini Dar es Salaam ni maalum kuziba nafasi za wagombea waliojiuzulu kwa wakati tofauti baada ya uchaguzi wa Juni 11 mwaka 2016.
  Waliojiuzulu ni aliyekuwa Mwenyekiti Yussuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Wajumbe wanne, Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah.
  Waliobaki katika Kamati ya Utendaji ni wane tu ambao ni Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay na Hussein Nyika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KADI ZA BENKI TU KUTUMIKA KWENYE UCHAGUZI WA YANGA JUMAPILI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top