• HABARI MPYA

  Sunday, January 06, 2019

  CHIRWA ASEMA KIU YAKE ITAISHA AKIIFUNGA NA YANGA ILIYOBAKI DAR

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Mzambia Obrey Chirwa, amesema kwamba atafurahi zaidi atakapokifunga kikosi kamili cha Yanga kilichobakia jijini Dar es Salaam.
  Kauli ya Chirwa imekuja muda mchache mara baada ya kufunga mabao mawili yaliyoiongoza Azam FC kuichapa Yanga mabao 3-0 jana Jumamosi kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, bao lingine kiliwekwa kimiani kwa mpira wa adhabu ndogo na Enock Atta-Agyei.
  Lakini kikosi cha Yanga kikionekana kuwa wachezaji mchanganyiko, wengi zaidi kutoka timu yao ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Yanga B.
  Obrey Chirwa amesema atafurahi zaidi atakapokifunga kikosi kamili cha Yanga kilichobakia mjini Dar es Salaam.

  “Mimi kila siku ninapofunga na kutoa pasi ya bao huwa najisikia raha tu, kwa sababu nafanya kazi na wenzangu, marafiki zangu, mimi siwezi kushinda peke yangu uwanjani, tunashinda kama timu na kupoteza kama timu, siwezi kucheza peke yangu uwanjani.
  “Kwa mimi kwa uwezo wangu nataka niifunge timu ile iliyoko Dar es Salaam, nitajua na kufurahi kuwa nishaifunga Yanga,” alisema mshambuliaji huyo aliyeiteketeza timu yake hiyo ya zamani.
  Kuelekea mechi mbili za mwisho za Kundi B la michuano hiyo dhidi ya KVZ na Malindi, alisema kuwa watahakikisha wanashinda mechi hizo, huku akigusia kuwa cha muhimu ni kufanya maandalizi vizuri wao kama wachezaji pamoja na benchi la ufundi.
  Aidha kwa kufunga mabao hayo, yamemfanya Chirwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaowania kuwa mfungaji wa michuano hiyo, akiwa na mabao mawili sawa na mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere.
  Chirwa pia hayo ndio mabao yake ya kwanza ya mechi za mashindano tokea asajiliwe na Azam FC kwenye usajili wa dirisha dogo mwezi uliopita, bao jingine alifunga katika mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 23 (Ngorongoro Heroes).
  Azam FC inatarajia kushuka tena dimbani kesho Jumatatu kuvaana na vinara wa Ligi Kuu Zanzibar, KVZ mchezo utakaofanyika Uwanja wa Amaan saa 10.15 jioni.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: CHIRWA ASEMA KIU YAKE ITAISHA AKIIFUNGA NA YANGA ILIYOBAKI DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top