• HABARI MPYA

    Wednesday, January 09, 2019

    AUSSEMS AWAENGUA KIKOSINI COULIBALY, KWASI MECHI NA SAOURA JUMAMOSI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mbelgiji wa Simba SC, Patrick J. Aussems amewaondoa kwenye programu ya mchezo dhidi ya JS Saoura mabeki Zana Coulibaly kutoka Burkina Faso na Mghana Asante Kwasi.
    Simba SC watakuwa wenyeji wa JS Saoura ya Algeria Jumamosi kuanzia Saa 10:00 jioni Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Na kuelekea mchezo huo, Aussems amewaweka pembeni wachezaji wanane – pamoja na Coulibaly na Kwasi, wengine ni kipa Ally Salim, mabeki Paul Bukaba, Yusuph Mlipili, kiungo Mohamed ‘Mo’ Ibrahim na washambuliaji Abdul Suleiman na Adam Salamba.

    Patrick Aussems amewaondoa Zana Coulibaly na Asante Kwasi kwenye mchezo dhidi ya JS Saoura

    Wanane hao wanabaki Zanzibar na wataungana na kikosi cha timu ya vijana, Simba B kuendelea na michuano ya Kombe la Mapinduzi kuanzia hatua ya Nusu Fainali.
    Wachezaji 18 wa Simba SC wamerejea leo Dar es Salaam kutoka Zanzibar baada ya timu kushinda mechi zote tatu za Kundi A Kombe la Mapinduzi, tayari kuendelea na maandalizi ya mchezo dhidi ya JS Saoura, klabu mpya ya mshambuliaji Mtanzania, Thomass Ulimwengu.
    Hao ni makipa; Aishi Manula na Deo Munishi ‘Dida’, mabeki Nicholas Gyan, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Pascal Wawa, viungo Jonas Mkude, James Kotei, Clatous Chama, Hassan Dilunga, Haruna Niyonzima, Said Ndemla, Muzamil Yassin, Shiza Kichuya, Rashid Juma na washambuliaji John Bocco, Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.
    Beki Erasto Nyoni ambaye ni majeruhi alirejea Dar es Salaam mapema juzi baada ya kuumia kwenye mchezo dhidi ya KMKM Jumapili.
    Viingilio katika mchezo wa Jumamosi ni Sh. 100,000 kwa watakaonunua tiketi za Platinum ambao watapatiwa huduma kukaa sehemu ya VIP A, Wataacha gari zao hoteli ya Serena na kuchukuliwa na basi maalum kwenda na kurudi Uwanja wa Taifa wakisindikizwa na Polisi, watapewa jezi mpya za Simba na Watapata viburudisho na vinywaji wakiwa uwanjani, Sh. 10,000 kwa VIP B na Sh. 5,000 kwa mzunguko.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AUSSEMS AWAENGUA KIKOSINI COULIBALY, KWASI MECHI NA SAOURA JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top