• HABARI MPYA

  Monday, December 03, 2018

  YANGA SC YATOKA NYUMA NA KUITANDIKA TANZANIA PRISONS 3-1 SOKOINE MRISHO NGASSA ATOLEWA KWA KADI NYEKUNDU

  Na Gwamaka Mwankota, MBEYA
  YANGA SC imetoka nyuma na kushinda 3-1 dhidi ya Tanzania Prisons jioni ya leo katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Ushindi huo unaifanya Yanga SC ifikishe pointi 38 baada ya kucheza mechi 14, ikiendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi tano zaidi ya Azam FC iliyo nafasi ya pili lakini imecheza mechi 13, wakati mabingwa watetezi, Simba SC wapo nafasi ya tatu kwa pointi zao 27 za mechi 12. 
  Haukuwa ushindi mwepesi kwa Yanga SC, kwani ililazimika kutoka nyuma baada ya kutanguliwa kwa kiungo Jumanne Elfadhil dakika ya 45 na ushei aliyefunga kwa penalti ya utata iliyotolewa na refa Meshack Suda wa Singida akimhukumu beki Andrew Vincent ‘Dante’ kufanya madhambi kwenye boksi.

  Dante alinusurika kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kichwa refa wakati wachezaji wa Yanga walipomvamia Suda kumtia kashikashi kupinga penalti hiyo.
  Kiungo wa Yanga SC, Mrisho Khalfan Ngassa na beki wa Tanzania Prisons, Laurian Mpalile wakatolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 45 na ushei baada ya kutwangana vichwa katika vurumai zilizohuissha karibu wachezaji wote.
  Filimbi ya kuhitimisha kipindi cha kwanza ilisaidia kutuliza jazba za wachezaji baada ya mawaidha waliyokwenda kupewa na walimu wao vyumbani na kipindi cha pili mchezo ulianza kwa utulivu.
  Prisons walifanikiwa kuwazuia Yanga kupata bao kwa nusu saa tu kabla ya mabadiliko ya kiufundi na weledi wa hali ya juu yaliyofanywa na kocha Mwinyi Zahera kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) kuwainua mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu.
  Aliwatoa viungo Maka Edward na Feisal Salum na kuwaingiza kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Matheo Anthony na baadaye akamtoa beki Juma Abdul na kumuingiza Amissi Joselyn Tambwe.
  Beki Nurdin Chona wa Tanzania Prisons akaunawa mpira kwenye boksi wakati akijaribu kumzuia mshambuliaji Mkongo, Heritier Makambo aliyepewa pasi na Tambwe na refa Suda akatenga penalti iliyokwenda kupachikwa nyavuni kiufundi na kiungo Ibrahim Ajibu Migomba dakika ya 76.
  Mrundi, Amissi Tambwe akawainua kwa shangwe wapenzi wa Yanga Uwanja wa Sokoine baada ya kufunga bao la pili kiufundi dakika ya 85 akimalizia pasi ya Matheo Anthony kabla ya kufunga tena la tatu dakika ya 90 na ushei.  
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, wenyeji Lipuli FC wameibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Biashara United ya Musoma mkoani Mara Uwanja wa Samora mjini Iringa, wakati Mwadui FC imelazimishwa sare ya 1-1 na KMC Uwanja wa Mwadui Complex mjini Shinyanga.  
  Kikosi cha Tanzania Prisons kilikuwa; Aaron Kalambo, Salum Kimenya, Laurian Mpalile, Nurdin Chona, James Mwasote, Jumanne Elfadhil, Benjamin Asukile, Cleophas Mkandala, Kelvin Friday, Hassan Kapalata na Jeremiah Juma/Hamisi Maingo dk83.
  Yanga SC; Ramadhani Kabwili, Juma Abdul/Amissi Tambwe dk72, Mwinyi Mngwali, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Feisal Salum ‘Fei Toto’/Thabani Kamusoko dk64, Mrisho Ngassa, Maka Edward/Matheo Anthony dk46, Heritier Makambo, Ibrahim Ajib na Raphael Daudi. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC YATOKA NYUMA NA KUITANDIKA TANZANIA PRISONS 3-1 SOKOINE MRISHO NGASSA ATOLEWA KWA KADI NYEKUNDU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top