• HABARI MPYA

    Friday, December 07, 2018

    YANGA INATISHA; MAKAMBO AWA MCHEZAJI BORA NA MWINYI ZAHERA KOCHA BORA WA LIGI KUU YA TANZANIA BARA MWEZI NOVEMBA 2018

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa timu ya Yanga ya Dar es Salaam, Heritier Makambo amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Novemba wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu wa 2018/2019.
    Makambo raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), alitwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda wenzake wawili, Said Dilunga wa Ruvu Shooting na beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’ wa Yanga alioingia nao fainali katika uchambuzi uliofanywa Dar es Salaam wiki hii na Kamati ya Tuzo ya TPL inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). 
    Kwa mwezi huo wa Novemba, Yanga ilicheza michezo minne, ambapo Makambo alitoa mchango mkubwa kwa Yanga kupata pointi 10  kwa ikishinda michezo mitatu na kutoka sare mmoja ikiwa nafasi ya kwanza, ambapo mshambuliaji huyo alifunga mabao matatu, huku Shaibu pia naye alitoa mchango mkubwa katika mafanikio hayo ya Yanga kwa mwezi huo hasa safu ya ulinzi na kuwa moja ya timu zenye ngome imara katika ligi msimu huu.
    Mwinyi Zahera (katikati) amekuwa Kocha Bora wa Mwezi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara

    Heritier Makambo amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Novemba wa Ligi Kuu Tanzania Bara 

    Kwa upande wa Dilunga naye alitoa mchango mkubwa kwa Ruvu Shooting akifunga mabao matatu katika michezo mitatu ambayo timu yake ilicheza ikishinda mmoja na kupoteza miwili.
    Pia Kamati ya Tuzo, imemchagua Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kuwa Kocha Bora wa Novemba akiwashinda Kocha Mkuu wa Coastal Union, Juma Mgunda na Kaimu Kocha Mkuu wa Alliance FC, Gilbert Dadi alioingia nao fainali. 
    Zahera aliiongoza timu yake kupata pointi 10 baada ya kushinda michezo mitatu na kutoka sare mmoja, ambapo Yanga iliifunga Mwadui mabao 2-1 mjini Shinyanga, ikaifunga Kagera Sugar mabao 2-1 mjini Bukoba na pia iliifunga JKT Tanzania mabao 3-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ilifungana bao 1-1 na Ndanda pia Dar es Salaam, hivyo Yanga kuwa kileleni mwa msimamo wa ligi. 
    Mgunda aliingia fainali kutokana na mafanikio ya Coastal Union kwa mwezi huo ikishinda michezo yote miwili iliyocheza, iliifunga Stand United mabao 2-1 ugenini mjini Shinyanga na iliifunga Ndanda bao 1-0 mjini Tanga na timu hiyo kushika nafasi ya sita katika msimamo, wakati Gilbert Dadi yeye aliingia hatua hiyo kutokana na mafanikio ya Alliance kwa mwezi huo, ambapo ilishinda michezo yote miwili iliyocheza na kuchupa kutoka nafasi ya 20 ambayo ni ya mwisho katika msimamo wa ligi hadi nafasi ya 17. 
    Alliance iliifunga Singida United bao 1-0 kisha pia iliifunga Mtibwa Sugar bao 1-0 mechi zote zikifanyika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza. 
    TFF ina utaratibu wa kuwazadiwa wachezaji bora wa kila mwezi, huku pia mwisho wa msimu kukiwa na tuzo mbalimbali zinazohusu ligi hiyo, ambapo msimu wa mwaka 2017/2018 kulikuwa tuzo 16 zilitolewa kwa washindi wa kada mbalimbali, ambapo kwa ushindi huo Makambo atazawadiwa tuzo, kisimbuzi kutoka Azam na sh. milioni moja. 
    Washindi wengine wa tuzo hiyo kwa msimu huu na miezi yao katika mabano ni mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere (Agosti), mshambuliaji wa Mbeya City, Eliud Ambokile (Septemba), mshambuliaji wa Simba Emmanuel Okwi (Oktoba).
    Kwa upande wa makocha walioshinda tuzo hizo kwa msimu huu ni Amri Said wa Mbao FC (Agosti), Mwinyi Zahera wa Yanga (Septemba) na Patrick Aussems wa Simba (Oktoba). 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA INATISHA; MAKAMBO AWA MCHEZAJI BORA NA MWINYI ZAHERA KOCHA BORA WA LIGI KUU YA TANZANIA BARA MWEZI NOVEMBA 2018 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top