• HABARI MPYA

  Wednesday, December 05, 2018

  TFF YATAMBUA KUREJEA MADARAKANI KWA WAMBURA? YAITISHA UCHAGUZI MDOGO BILA KUHUSISHA NAFASI YA UMAKAMU WA RAIS

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KUASHIRIA kumtambua Michael Richard Wambura kama Makamu wa Rais, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limesitisha mpango wa uteuzi wa mtu mpya katika nafasi hiyo.  
  Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Mario Ndimbo amewaambia Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam kwamba, Kamati ya Uchaguzi ya shirikisho imetangaza uchukuaji fomu za uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi zilizo wazi.
  Ndimbo amezitaja nafasi hizo ni za Mjumbe Kamati ya Utendaji kuwakilisha Lindi na Mtwara na Mjumbe Kamati ya Utendaji kuwakilisha Simiyu na Shinyanga.
  Ndimbo amesema kwamba zoezi la kuchukua na kurudisha fomu lilianza jana na litafikia tamati Jumapili wiki hii na kwamba fomu zinapatikana makao makuu ya TFF, Uwanja wa Karume, Ilala mjini Dar es Salaam au kwenye tovuti ya shirikisho kwa gharama ya Sh. 200,000 kwa nafasi moja na malipo yote yatapitia benki.

  Rais wa TFF, Wallace Karia (kulia) na Makamu wake, Michael Wambura (kushoto)

  Novemba 30, mwaka huu Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam ilitengua maamuzi ya Kamati za Maadili za TFF kumfungia maisha Wambura kujihusisha na soka kufuatia kesi aliyofungua kupinga maamuzi hayo.
  Kwa uamuzi huo, Wambura anarejea katika madaraka yake ya Umakamu wa Rais wa TFF na Uenyekiti wa Chama cha Soka Mara (FAM).
  Maana yake, Athumani Nyamlani aliyekuwa anakaimu nafasi hiyo sasa anapoteza wadhifa huo aliopewa baada ya kuwa Mjumbe Mteule wa Kamati ya Utendaji. 
  Katika kesi hiyo TFF, iliyo chini ya Rais Wallace Karia ilikuwa inawakilishwa Wakili David Ndosi, ambaye hata hivyo leo hakuonekana wakati wa hukumu. Nakala za hukumu zinatarajiwa kuwafikia TFF mapema Jumatatu.
  Machi mwaka huu Kamati ya Maadili ya TFF chini ya Mwenyekiti wake, Hamidu Mbwezeleni ilimfungia maisha Wambura kutojihusisha na masuala ya soka kwa kumtuhumu kwa makosa matatu.
  Katika taarifa yake, TFF ilisema kwamba ilichukuwa hatua hiyo kwa mujibu wa kifungu cha 73(1) (c) cha Kanuni za Maadili ya TFF Toleo la 2013. 
  Hiyo ni baada ya kikao chake cha Machi 14, mwaka huu ambacho pamoja na mambo mengine, kilimjadili Wambura aliyefikishwa kwenye Kamati hiyo kwa tuhuma za makosa matatu ya kupokea fedha za TFF malipo yasiyo halali, kugushi  barua na kushusha hadhi ya TFF.
  Wambura alifikishwa kwenye Kamati ya Maadili na Sekretarieti ya TFF iliyodai baada ya Kamati ya Ukaguzi kukutana na kupitia mambo mbalimbali ya ukaguzi na suala hilo la Wambura ilionekana linatakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili.
  Ikumbukwe Wambura alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa TFF Agosti 12, mwaka jana mjini Dodoma katika uchaguzi uliomuweka madarakani Karia katika nafasi ya Urais.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TFF YATAMBUA KUREJEA MADARAKANI KWA WAMBURA? YAITISHA UCHAGUZI MDOGO BILA KUHUSISHA NAFASI YA UMAKAMU WA RAIS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top