• HABARI MPYA

    Tuesday, December 11, 2018

    SIMBA SC WAONDOKA NA WACHEZAJI 20 KESHO KUIFUATA NKANA FC, MECHI KUCHEZESHWA NA WANIGERIA JUMAPILI KITWE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha Simba SC kinatarajiwa kuondoka kesho kwenda Zambia kwa ajili ya mchezo wa kwanza hatua ya mwisho ya mchujo ya kuwania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Nkana FC.
    Mchezo umepangwa kufanyika Uwanja wa Nkana mjini Kitwe nchini Zambia kuanzia Saa 7:00 mchana ukichezeshwa na refa Salisu Basheer atakayesaidiwa na washika vibendera Peter Eigege Ogwu na Efosa Celestine Igudia wote wa Nigeria.
    Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Hajji Sunday Manara amesema kwamba kikosi kitaondoka Saa 10:00 Alfajiri kwa ndege ya shirika la Ethiopia kikiwa na wachezaji 20, maofisa sita wa Benchi la ufundi wakiongozwa na Kocha Mkuu, Mbelgiji Patrick Aussems pamoja na viongozi watatu.

    Manara amesema kwamba msafara utaongozwa na Mjumbe wa kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Francis Ndulane.
    “Simba itaelekea Zambia kwa ndege ya Shirika la ndege la Ethiopia kwa kupitia Addis Ababa na kisha Mjini Ndola nchini Zambia, kisha itaunganisha moja kwa moja Kwenye Mji wa Kitwe ambapo mchezo huo ndipo unapotarajiwa kuchezwa Siku ya Jumapili jioni.
    Manara pia amesema kwamba msafara wa mashabiki wa timu hiyo utaondoka Alfajiri ya Alhamisi kwa basi la klabu kupitia Tunduma Jijini Mbeya na kufika Kitwe Ijumaa jioni.
    Kila shabiki anayesafiri amelazimika kulipa kiasi cha Sh. 130,000 kwa safari ya kwenda Kitwe nchini Zambia na kurudi Dar es Salaam.
    Simba SC imefika hatua hii baada ya kuitoa Mbabane Swallows ya eSwatini, zamani Swaziland kwa jumla ya mabao 8-1, ikishinda 4-1 Dar es Salaam na 4-0 Manzini, wakati Nkana FC imeitoa UD Songo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 3-1, ikishinda 2-1 mjini na 1-0 Kitwe.
    Baada ya mechi ya kwanza Jumapili hii mjini Kitwe nchini Zambia, mchezo wa marudiano utafuatia Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam Desemba 23. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC WAONDOKA NA WACHEZAJI 20 KESHO KUIFUATA NKANA FC, MECHI KUCHEZESHWA NA WANIGERIA JUMAPILI KITWE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top