• HABARI MPYA

  Sunday, December 09, 2018

  MIAKA 57 YA UHURU TANZANIA BADO ‘KICHWA CHA MWENDAWAZIMU’

  LEO ni miaka 57 tangu taifa letu lipate Uhuru wake na kupandisha bendera yake wakati huo Tanganyika, kabla ya Muungano na ndugu zetu wa Zanzibar uliozaa Jamhuri tukufu ya Muungano wa Tanzania.
  Huwezi kuzungumzia Uhuru wan chi yetu bila kumtaja marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, baba wa taifa hili.
  Mwalimu Nyerere ni Rais wa kwanza na muasisi aliyeliletea taifa hili uhuru wa kweli kutoka kwenye makucha ya mkoloni Desemba 9, mwaka 1961. 

  Mwalimu Nyerere alizaliwa Aprili 13, mwaka 1922 katika kijiji kidogo cha mwitongo huko Butihama, kasikazini mwa Tanzania karibu kabisa na ziwa Victoria, akiwa mtoto wa Chifu Burito Nyerere wa kabila dogo la Wazanaki
  Mwalimu Nyerere alifariki dunia kwa ugonjwa wa saratani ya damu, siku ya Alhamisi Oktoba 14, mwaka 1999 saa 4:30 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki, katika hospitali ya Mtakatifu Thomas London nchini Uingereza akiwa amezungukwa na timu ya madaktari bingwa.
  Enzi za uhai wake, mwaka 1988, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere akiwa bado ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi alialikwa kama mgeni rasmi wa maadhimisho ya miaka 11 ya CCM ambayo yalifanyika Kitaifa Mkoani Tabora.
  Katika Hotuba yake, Mwalimu Nyerere aliwakumbusha wazee wa Tabora na kuwashukuru kwa moyo wao wa kujitolea, Mwalimu alisema isingelikuwa kwa ujasiri wao, tusingelikuwa na Tanzania huru.
  Mwalimu aliutaja mji wa Tabora kama kitovu kikuu cha harakati zake, akisema kuwa aliishi Tabora miaka tisa, akiwa mwanafunzi Tabora School kwa miaka sita na baadaye Mwalimu wa shule ya Saint Mary's kwa miaka mitatu. 
  Alisema aliishi Tabora wakati wa Vita na wakati wa Amani na alijifunza kucheza bao katika viunga vya mji huo akiwa bado ni mwanafunzi bali akitoka kanisani alikuwa akienda kwenye vijiwe vya wazee na kucheza nao bao.
  Mwalimu Nyerere alisema alijifunza hekima, busara nyingi na namna ya kuishi na watu kutoka kwa wazee hao.
  Hali halisi ya sasa katika sekta ya michezo nchini imenikumbusha kuhusu hotuba hii ya Mwalimu katika maadhimisho ya miaka 11 ya CCM ambayo yalifanyika Kitaifa Mkoani Tabora.
  Michezo nchini imekuwa ikishuka kwa kasi mno siku hadi siku na kuzidi kupoteza ladha na msisimko wake.
  Enzi za Mwalimu Nyerere Tanzania ilisifika kwa michezo mbalimbali – pamoja na soka kulikuwa kuna Riadha, Ngumi na kote huko nchi iliibua magwiji wa kutosha akina Sulieman Nyambui, Juma Ikangaa, Filbert Bayi, Titus Simba, Habib Kinyogoli, Emmanuel Mlundwa, Omar Mahadhi, Abdallah Kibadeni, Maulid Dilunga na Sunday Manara.
  Na hata klabu zetu zilifanya vyema katika michuano ya Afrika wakati huo na kutabiriwa kuja kuwa tishio zaidi baadaye.
  Lakini maendeleo ya kimichezo, au mafanikio hayakuishia uwanjani tu, yalionekana hadi nje ya Uwanja ikishuhudiwa klabu zikisimamisha majengo ya thamani na kununua magari. Miaka ya 1970, klabu za Simba na Yanga ziliweza kujiendesha kutokana na rasilimali zake. 
  Hali ni tofauti mno hivi sasa, majengo yamechakaa na kwa Yanga iliyokuwa na jengo zaidi ya moja limebaki moja la makao makuu pale Jangwani ambalo hata hivyo hawaishi watu.
  Kwa ujumla mambo yamekuwa tofauti mno na ilivyotarajiwa, michezo nchini inazidi kudumaa kila kukicha na ilipofikia inakatisha tamaa, kiasi kwamba twendako ni kiza kinene.
  Haya ni matunda ya viongozi wa sasa ambao wametengeneza mfumo unaowaweka kando wazee na kwa ujumla wapenzi halisi wa michezo kwa kigezo cha elimu. 
  Kwa zaidi ya miaka 10 sasa michezo nchini, hususan soka inaongozwa na wasomi wa kiwango cha juu na kwenye Katiba zao wameweka wazi hawataki watu ambao wana elimu chini ya Kidato cha Nne, ingawa hao ndiyo wenye mapenzi ya dhati ya michezo. 
  Viongozi wasomi wa leo hawaoni cha maana kwa wazee au waasisi wa klabu, wakati Mwalimu Nyerere alisema alijifunza hekima, busara nyingi na namna ya kuishi na watu kutoka kwa wazee wa Tabora. Unaweza kuona kwa nini Mwalimu Nyerere aliweza, na kwa nini michezo inazidi kuporomoka kila kukicha nchini na hata baada ya miaka 57 ya Uhuru, Tanzania bado kichwa cha mwendawazimu kama alivyowahi kusema Rais wa pili wa nchi hii, Mzee Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MIAKA 57 YA UHURU TANZANIA BADO ‘KICHWA CHA MWENDAWAZIMU’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top