• HABARI MPYA

    Saturday, December 08, 2018

    KAMATI YA UCHAGUZI YA TFF YAMUENGUA MGOMBEA ALIYETAKA KUGOMBEA UENYEKITI NA UMAKAMU KWA MPIGO YANGA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imemuengua Yono Kevela katika uchaguzi wa Yanga SC uliopangwa kufanyika Januari 13 mwakani kwa sababu ya kuomba nafasi mbili kwa mpigo.
    Taarifa ya Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Mario Ndimbo imesema kwamba mmiliki huyo wa kampuni maarufu ya minada, Yono Auction Mart Limited aliomba nafasi mbili, Uenyekiti na Umakamu katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Januari 13 mjini Dar es Salaam maalum kuziba nafasi za wagombea waliojiuzulu kwa wakati tofauti baada ya uchaguzi wa Juni 11 mwaka 2016.
    Sasa Kamati imepitisha wagombea wawili katika nafasi ya Uenyekiti, Mbaraka Igangula na Jonas Tiboroha baada ya kumuengua pia na Erick Mlinga kufuatia taarifa zake alizojaza kwenye fomu kutofautiana na nyaraka halisi.
    Yono Kevela (kulia) ameenguliwa kwenye uchaguzi wa Yanga kwa kuomba nafasi mbili kwa mpigo

    Katika usaili uliofanyika kwa siku tatu kuanzia Alhamisi makao makuu ya TFF, Uwanja wa Karume Ilala, mjini Dar es Salaam, kwenye nafasi ya Makamu Mwenyekiti waliopitishwa ni watatu ambao ni Titus Osoro, Pindu Luhoyo na Salum Magege Chota.
    Na kwenye nafasi ya Ujumbe waliopitishwa ni Athanas Kazighe, Ramadhan Said, Salim Rupia, Dominic Francis, Shafii Amri, Benjamin Mwakasonda, Christopher Kashiririka, Ally Msigwa, Sylvester Haule, Arafat Hajji,  Frank Kalokole na Said Kambi.
    Wagombea wane, Hamad Islam, Seko Kongo, Leonard Marango na Benard Mabula hawakufika kwenye usaili na kwa mujibu wa kanuni wameenguliwa katika uchaguzi na Ndimbo amesema wagombea ambao hawakupitishwa wana haki ya kukata rufaa Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ya TFF.
    Ndimbo amesema kwamba Kamati itatangaza matokeo ya usaili na kutaja orodha ya mwisho ya wagombea waliopitishwa, kabla ya kupelekea masuala ya Kimaadili kwa Sekretarieti ya TFF, ambayo itayawasilisha Kamati ya Maadili kati ya Desemba 11 hadi 14 Kamati.
    Kamati ya Maadili itatangaza uamuzi wa masuala ya Kimaadili iliyoyajadili Desemba 14, kabla ya kutoa fursa ya wagombea walioathirika na zoezi hilo kukata Rufaa na Januari 4 hadi 6 orodha kamili ya mwisho ya wagombea itatolewa baada ya michakato yote tayari kwa kampeni kati ya Januari 8 na 12.
    Viongozi waliojiuzulu Yanga baada ya uchaguzi wa Juni 11 mwaka 2016 ni aliyekuwa Mwenyekiti Yussuf Manji, Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Wajumbe wanne, Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah.
    Waliobaki katika Kamati ya Utendaji ni wane tu ambao ni Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay na Hussein Nyika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMATI YA UCHAGUZI YA TFF YAMUENGUA MGOMBEA ALIYETAKA KUGOMBEA UENYEKITI NA UMAKAMU KWA MPIGO YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top