• HABARI MPYA

  Tuesday, December 11, 2018

  KAMATI YA MAADILI YA TFF YAWAFUNGIA VIONGOZI ARFA KWA UBADHIRIFU WA FEDHA ZA MECHI YA SIMBA NA ARUSHA UNITED

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imewafungia kujihusisha na soka viongozi wanne wa Chama cha Soka Arusha (ARFA) kwa tuhuma za kufanya ubadhirifu wa mapato ya mchezo kati ya Arusha United na Simba SC uliofanyika Agosti 15, mwaka huu Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. 
  Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Mario Ndimbo amesema kwamba katika kikao chake cha Novemba 5 na 7, mwaka huu, Kamati hiyo ilipitia shauri linalowakabili viongozi hao wa ARFA ambao ni Peter Temu (Mwenyekiti), Mwarizo Nassoro, (Katibu Msaidizi), Omary Nyambuka (Mweka Hazina) na Hamisi Issa (Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF).
  Kwa pamoja, wane hao walishtakiwa na Sekretarieti ya TFF kwa mashtaka 4 ambayo ni; kupokea/kuchukua isivyo kihalali fedha za TFF kiasi cha shilingi za kitanzania 1,205,808 za mgao wa mapato ya mechi ikiwa ni kinyume na kifungu cha 13[4] na 73[1] [a] Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
  Kupokea/kuchukua isivyo kihalali fedha za BMT kiasi cha shilingi za kitanzania 241,161 za mgao wa mapato ya mechi ikiwa ni kinyume na kifungu cha 13[4] na 73[1] [a] kanuni za maadili za TFF toleo la 2013.
  Rais wa TFF, Wallace Karia (kulia) na Katibu wake, Wilfred Kidau wametolea ufafanuzi tuhuma za ubadhirifu wa Sh. Milioni 300
  Kupokea/kuchukua isivyo kihalali fedha za VAT [kodi] kiasi cha shilingi za kitanzania 5,174,084 za mgao wa mapato ya mechi ikiwa ni kinyume na kifungu cha 13[4] na 73[1] [a]kanuni za maadili za TFF toleo la 2013.
  Kupokea / kuchukua isivyo kihalali fedha za gharama za uwanja kiasi cha shilingi za kitanzania 1,373,745 za mgao wa mapato ya mechi ikiwa ni kinyume na kifungu cha 13[4] na 73[1] [a] kanuni za maadili za TFF toleo la 2013.
  Peter Temu (Mwenyekiti ARFA) alishtakiwa na Sekretarieti ya TFF kwa mashtaka 2 ambayo ni; Kushindwa kutekeleza majukumu yake kama msimamizi wa kituo kinyume na kifungu cha 49[19] cha kanuni za ligi kuu toleo la 2013.
  Ubadhirifu, kughushi, kuongopa na kuiba kinyume na kanuni ya 13[4] na kanuni ya 73(7) za kanuni za maadili za TFF toleo la 2013.
  Baada ya kulipitia shauri hilo ikiwa pamoja na kuwaita na kuwasikiliza washtakiwa ambao walichagua utetezi kwa njia za kufika kwenye kikao na wengine wawili wakiwasilisha utetezi wao kwa njia ya maandishi.
  Kamati imejiridhisha kuwa watuhumiwa wote 4, wakiwa viongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Arusha (ARFA), wameshindwa kusimamia mapato ya mchezo kati ya Arusha United na Simba SC uliofanyika siku ya Jumatano tarehe 15 Agosti 2018 katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha. Badala ya kuwa mstari wa mbele katika kudhibiti mapato ya mchezo huo, viongozi hao walihusika moja kwa moja na upotevu wa fedha hizo. Kwa makosa hayo, Kamati inatoa adhabu zifuatazo;
  Peter Temu - Mwenyekiti ARFA, akiwa Msimamizi wa Kituo siku ya mchezo alishindwa kusimamia majukumu yake ipasavyo, na hivyo fedha kuchukuliwa kiholela bila kufuata utaratibu. Vile vile alishindwa kutoa maelezo ya matumizi ya fedha alizochukua kutoka katika mgao huku akifahamu fika kuwa hiyo siyo kazi yake. Kwa makosa hayo;
  Kamati inamfungia kutojihusisha na masuala ya mpira maisha ndani na nje ya nchi. Adhabu hii inatolewa kwa mujibu wa kifungu cha 73(1)(c) & (7) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
  Kamati imeiomba Sekretarieti ya TFF ihakikishe kuwa Ndugu Temu anarejesha fedha zote alizochukua na kushindwa kuzitolea maelezo, hasa fedha za makato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
  Mwarizo Nassoro - Katibu Msaidizi wa ARFA, alishindwa kutoa maelezo ya fedha alizopokea kutoka katika mgao wa mapato. Vile vile hakufanya mawasilisho ya fedha hizo kwenye tasisi husika. Nasoro alipokea fedha hizo huku akifahamu fika kuwa kazi hiyo inatakiwa kufanywa na Mweka Hazina. Kwa makosa hayo;
  Kamati inamfungia kutojihusisha na masuala ya mpira maisha ndani na nje ya nchi. Adhabu hii inatolewa kwa mujibu wa kifungu cha 73(1)(c) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
  Kamati inaiomba Sekretarieti ya TFF ihakikishe kuwa Ndugu Nassoro anarejesha fedha zote alizochukua na kushindwa kuzitolea maelezo, hasa fedha za makato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).
  Hamisi Issa (Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ARFA na Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF) aliingilia majukumu ya Mweka Hazina kwa kupokea fedha za gharama za mchezo. Issa alishindwa kutoa uthibitisho wa matumizi ya fedha hizo. Kwa makosa hayo;
  Kamati inamfungia kutojihusisha na masuala ya mpira ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miaka 5. Adhabu hii inatolewa kwa kwa mujibu wa kifungu cha 73(1)(a)(ii) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
  Kamati imeiomba Sekretarieti ya TFF ihakikishe kuwa Hamisi Issa anarejesha fedha zote alizochukua na kushindwa kuzitolea maelezo. 
  Omary Nyambuka (Mweka Hazina wa ARFA) alishindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Aidha Nyambuka hakutoa taarifa kwa vyombo husika baada ya kuona anaingiliwa katika majukumu yake. Hivyo kwa kosa hilo Kamati inamfungia kutojihusisha na masuala ya mpira ndani na nje ya nchi kwa kipindi cha miaka 5. Adhabu hii imetolewa chini ya kifungu cha 6(1)(h) cha Kanuni za Maadili za TFF toleo la 2013.
  Kamati imeiomba Sekretarieti ya TFF kupeleka suala hili kwenye vyombo vya dola, ili hatua zaidi zichukuliwe kwa mujibu wa sheria za nchi. Hii itasaidia kupunguza wimbi la ubadhirifu, wizi na upotevu wa mapato unaofanywa na baadhi ya viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza mpira nchini. Aidha Kamati inaishauri Sekretarieti kuimarisha mfumo wa usimamizi wa mapato ya michezo kwa kuhakikisha kunakuwa na ufuatiliaji wa mara kwa mara wa taarifa za mapato ili kuongeza uwajibikaji kwa wasimamizi wa vituo; hii ni pamoja na kukiongezea uwezo Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani.
  Wakati huo huo: TFF imezungumzia tuhuma za ubadhirifu wa fedha, zaidi ya Sh. Milioni 300 zinazowakabili ikidai zinatokana na Taarifa ya Hesabu za TFF za mwaka 2015 na 2016 zilizopokelewa Septemba 11, mwaka 2016 Novemba 27 mwaka 2017 kwa mfuatano na kufanyiwa kazi.
  Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Mario Ndimbo amesema kwamba katika kipindi hicho kilichotajwa kimekuwa chini ya ukaguzi wa PCCB na tayari mashauri yako mahakamani yanaendelea ikiwa ni pamoja na kufuatilia waliotajwa katika hesabu za fedha katika kipindi cha mwaka 2015 na 2016.
  “Kwa kuwa masuala hayo yapo kwenye ngazi ya mahakama, TFF inaona  iviachie vyombo vya kisheria vifanye kazi yake kadiri ya taratibu zao,”imesema taarifa ya Ndimbo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KAMATI YA MAADILI YA TFF YAWAFUNGIA VIONGOZI ARFA KWA UBADHIRIFU WA FEDHA ZA MECHI YA SIMBA NA ARUSHA UNITED Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top