• HABARI MPYA

  Sunday, December 09, 2018

  ALLY KIBA ASABABISHA KONA ILIYOZAA BAO COASTAL UNION YATOA SARE 1-1 NA MBEYA CITY MKWAKWANI

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  TIMU ya Coastal Union ya Tanga imelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga jioni ya leo.
  Kwa matokeo hayo, timu hizo zinaendelea kufuatana katika nafasi yano tano na sita, zote zikifikisha pointi 23, Mbeya City baada ya kucheza mechi 16 na Coastal Union mechi 15.
  Katika mchezo wa leo, Coastal Union walitangulia kwa bao la mshambuliaji Ayoub Lyanga dakika ya tano akimalizia kwa kichwa mpira wa kona iliyopigwa na kiungo mkongwe, Athumani Iddi ‘Chuji’.
  Na kona hiyo iliyosababishwa na mshambuliaji mpya wa timu hiyo, mwanamuziki Ally Kiba aliyekuwa anacheza kwa mara ya kwanza tangu asajiliwe msimu huu.

  Ally Kiba (kulia) leo ameanza Coastal Union na kusababisha kona iliyoipa bao timu yake

  Kiba aliyedumu uwanjani kwa dakika 64 kabla ya kumpisha Deo Anthony, alicheza vizuri na kwa uelewano na wenzake ingawa hakupata muda wa kutosha wa kufanya nao mazoezi kutokana na shughuli zake za muziki.
  Mbeya City ilisawazisha bao hilo dakika ya 50 baada ya Bakari Mwamnyeto kujifunga katika harakati za kuokoa dhidi ya mshambuliaji Victor Hangaya. 
  Mechi nyingine ya Ligi Kuu inafuatia hivi sasa kati ya Yanga SC na Biashara United Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Kikosi cha Coastal Union kilikuwa; Hussein Sharrif ‘Casillas’, Mbwana Hamisi ‘Kibacha’, Abdallah Waziri, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Ame Mohammed, Athumani Iddi ‘Chuji’/Hassan Mwangayamba dk54, Issa Abushehe/Mohamed Mussa ‘Kijiko’ dk50, Mtenje Albano, Andrew Simchimba, Ally Kiba/Deo Anthony dk64 na Ayoub Lyanga.
  Mbeya City; Fikirini Bakari, Kabanda, Mpoki Mwakinyuki, Ibrahim Ndunguri, Ally Lundenga, Medson Mwakatundu, Iddi Suleiman ‘Nado’, Mohammed Samatta, Victor Hangaya/Godfrey Mulla dk89, Ramadhani Kapenta na Eliud Ambokile.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ALLY KIBA ASABABISHA KONA ILIYOZAA BAO COASTAL UNION YATOA SARE 1-1 NA MBEYA CITY MKWAKWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top