• HABARI MPYA

  Thursday, November 15, 2018

  SIMBA SC YAPANIA KUMFURAHISHA RAIS DK JPM KWA KUFANYA VIZURI LIGI YA MABINGWA AFRIKA

  Na Nasra Omary, DAR ES SALAAM
  BAADA ya rais John Pombe Magufuli kutoa agizo  kwa timu za Tanzania kufanya vizuri kwenye  michuano ya Afrika, Simba inayoshiriki Ligi ya  Mabingwa imeonesha dhamira yake ya  kufanya vizuri kwenye mashindano hiyo. 
  Simba watashuka dimbani Novemba 28 kwenye  mchezo wao wa kwanza dhidi ya Mabingwa wa  eSwatini, zamani Swaziland, Mbabawe Swallows kwenye uwanja wa  Taifa,  Dar es Salaam. 
  Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar  es Salaam, Ofisa Habari wa timu ya Simba Hajji Manara alisema kuwa wamepewa maagizo na Rais  Magufuli kuhakikisha wanakuwa mabingwa wa  Afrika kwenye michuano hiyo na watahakikisha  wanafanya vizuri. 
  Amesema kuwa wanaajua ugumu wa kupata  ubingwa kwenye Afrika lakini wanadhamira na  dhamira yao ya kwanza ni kuhakikisha wanaingia  kwenye hatua za makundi kwenye mashindano  hayo.

  Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli anataka timu za Tanzania zifanye vizuri kwenye mashindano ya kimataifa  

  Alisema kuwa kama Mungu akiwajaalia wakaingia  kwenye hatua hiyo ya makundi lolote linaweza  kutokea kuanzia hapo.
  "Tukifanikiwa kufuzu kuingia kwenye hatua za  makundi basi tunaweza kufika popote, tuajua  haitakuwa rahisi lakini tutahakikisha tunapambana  ili tufike mbali zaidi," Alisema Manara
  Manara alisema kuwa Mbabawe Swallows, siyo  timu rahisi ya kuibeza  na ndio maana tunajipanga ili  kuhakikisha tunashinda mchezo huo.
  Amesema kuwa watahakikisha wanautumia vyema  uwanja wa nyumbani kwa kupata ushindi mnono ili   wakienda kwenye mchezo wa marudiano wawe na  rekodi nzuri.
  Hata hivyo Manara amesema kuwa kikosi chao  kinatarajiwa kushuka dimbani Novemba 16, Ijumaa  kuvaana na mabingwa wa Malawi, Big Bullets,  kwenye mchezo wa kirafiki utakaochezwa Uwanja  wa Taifa Dar es Salaam kuanzia saa 12 jioni.
  Manara alisema kiingilio katika mchezo huo  kitakuwa sh. 3,000, sh. 7,000 na sh. 10,000,  aliwaomba mashabiki wa Simba kumwagika kwa  wingi uwanjani hapo kuishangilia timu yao.
  "Mchezo wetu huu na wa  Ligi dhidi ya Lipuli FC  tutakaocheza Novemba 21, tutautumia vyema  kama sehemu ya maandalizi ya mchezo dhidi ya  Mbabane, tunaamini mwalimu atayafanyia kazi  mapungufu atakayoyaona kwenye mchezo huo  kabla ya kukutana na mabingwa hao wa Swaziland,"  alisema.
  Ni miaka saba tangu Simba irejee tena kwenye  michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo mara  ya mwisho walishiriki mwaka 2003, walipofanikiwa  kufika hatua ya makundi ya michuano ya kimataifa  baada ya hapo wakapotea kabla ya kutwaa ubingwa  msimu uliopita.
  Swallows kwao ni mara ya pili mfululizo kushiriki  michuano hii ambapo msimu uliopita waliishia  hatua ya makundi sasa wamerejea tena kwenye  michuano hiyo.
  Simba walichukua Ubingwa baada ya kucheza  michezo 30 wakiwa na Pointi 69 baada ya kutoa  sare michezo tisa na kupoteza mchezo mmoja huku  wakishinda michezo 20. 
  Kama Simba watapita hatua hiyo ya awali ya Ligi ya  Mabingwa Afrika,  raundi ya kwanza watakutana na  mshindi kati ya Nkana Rangers ya Zambia dhidi ya  Uniao Desportiva Do Songo ya Mozambique.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAPANIA KUMFURAHISHA RAIS DK JPM KWA KUFANYA VIZURI LIGI YA MABINGWA AFRIKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top