• HABARI MPYA

    Monday, November 12, 2018

    SIMBA SC KUMENYANA NA BIG BULLETS YA MALAWI IJUMAA MECHI YA KIRAFIKI KUJIANDAA NA MBABANE SWALLOWS LIGI YA MABINGWA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAWAKILISHI wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba SC Ijumaa wiki hii watamenyana na Big Bullets FC ya Malawi katika mchezo wa kirafiki utakaofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Mchezo huo ni maalum kwa kocha Mbelgiji, Patrick J Aussems kukipima kikosi chake kabla ya mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Mbabane Swallows ya eSwatini, zamani Swaziland utakaofanyika kati ya Novemba 27 na 28 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Ikifanikiwa kuvuka mtihani huo baada ya mchezo wa marudiano kati ya Desemba 4 na 5, mwaka huu eSwatini – Simba itamenyana na mshindi kati ya UD Songo ya Msumbiji na Nkana FC ya Zambia, anayochezea beki wake wa zamani, Mtanzania, Hassan Kessy aliyewahi kucheza na Yanga pia katika raundi ya pili ya mchujo.

    Katika droo ya michuano ya klabu barani Afrika iliyotajwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), wawakilishi wa Zanzibar, JKU watamenyana na Al Hilal ya Sudan na mshindi baina yao atakutanana mshindi kati ya APR FC ya Rwanda na Club Africain ya Tunisia. 
    mechi za kwanza za raundi ya pili ya pili na ya mwisho ya mchujo zitachezwa kati ya Desemba 14 na 16 na marudiano Desemba 21 na 23, mwaka huu.
    Katika Kombe la Shirikisho, Mtibwa Sugar itaanza na Northern Dynamo ya Shelisheli na ikivuka mtihani huo itakutana na K.C.C.A ya Uganda.
    Wawakilishi wa Zanzibar, Zimamoto wamepewa kigongo, Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na mshindi baina yao atakutana na mshindi kati ya El Geco ya Madagascar na Deportivo Unidad ya Equatorial Guinea.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC KUMENYANA NA BIG BULLETS YA MALAWI IJUMAA MECHI YA KIRAFIKI KUJIANDAA NA MBABANE SWALLOWS LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top