• HABARI MPYA

    Tuesday, November 13, 2018

    MBAO FC WAINGIZWA MICHUANO YA SPORTPESA SUPER CUP 2019 BAADA YA KUIPIGA SIMBA SC 1-0 KIRUMBA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BAADA kuitandika Simba 1-0 hivi karibuni katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, timu ya Mbao FC imejumuishwa kwenye orodha ya timu zitakazoshiriki michuano ya SportPesa Super Cup mwakani.
    Michuano ya SportPesa Super Cup ni ligi ya mpira wa miguu inayoshirikisha timu nane na kuchezwa kwa mtoano ambapo awamu ya tatu ya michuano itachezwa Januari 2019 na kushirikisha timu kutoka Kenya na Tanzania. 
    Michuano ya SportPesa Cup ilizinduliwa Tanzania 2017 huku mshindi wa mashindano hayo, Gor Mahia kutoka Kenya akicheza na timu ya Everton kutoka England kwenye uwanja wa Taifa hapa jijini Dar es Salaam 2018, kwenye awamu ya pili ya michuano hiyo ilichezwa Nakuru, Kenya huku timu ya Gor Mahia kwa mara nyingine ikiibuka mshindi wa michuano ambapo ilisafiri nchini Uingereza na kucheza na timu ya Everton siku ya Jumanne ya Novemba 6, mwaka huu.

    Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti SportPesa Tanzania, Tarimba Abbas (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam

    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam wakati wa kutangaza awamu ya tatu ya michuano hiyo, Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti SportPesa Tanzania Tarimba Abbas alisema kuwa tangu kuzinduliwa kwa michuano hiyo miaka mitatu iliyopata, SportPesa Cup imekuwa ikipata mafanikio makubwa kutoka mwaka hadi mwaka na kuvuta maelfu ya mashabiki ukizingatia kwamba bingwa wa mashindano hayo amekuwa akicheza na moja ya timu kubwa inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uingereza – Everton FC.
    “Michuano hii imekuwa na mafanikio makubwa na imeweza kusaidia kuinua kiwango cha klabu pamoja na wachezaji wetu. Kama mnavyofahamu, ni kupitia SportPesa Super cup ambapo timu inayoshiriki Ligi Kuu nchini Uingereza iliweza kutengeza historia kwa mara ya kwanza kuja kucheza hapa uwanja wetu wa Taifa jijini Dar es Salaam. 
    Vile vile, ni kwa mara ya kwanza kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki kutoa timu ambayo ni Gor Mahia kwenda kucheza mechi ya ushindani nchini Uingereza. Mbali na timu ya Gor Mahia kupoteza mchezo huo, lakini nina uhakika wachezaji wameweza kujiongezea ujuzi ambao nina uhakika utabadilisha kiwango na hamasa ya mpira soka kwenye ukanda wetu huu, alisema Tarimba.
    Tarimba alisema michuano ya 2019 itashirikisha timu za Simba, Yanga, Singida United na Mbao kutoka Tanzania pamoja na Gor Mahia, Kariobangi Sharks, Bandari FC na AFC Leopards kutoka Kenya. Tarimba aliongeza kuwa timu tatu kutoka Afrika Mashariki ambazo zitatajwa baadae zitashiriki kama timu waalikwa.
    Mshindi wa michuano ya SportPesa Super cup 2019 atajishindia kitita cha USD 30,000 lakini la muhimu atacheza na timu ya Everton FC kutoka Uingereza. Mshindi wa pili atajishindia USD 10,000, wa tatu USD 7,500 huku wanne akinyakulia kitita cha USD 5,000 alisema Tarimba huku akiongeza kuwa timu ambayo itafanikiwa kufika robo kila moja ikijishindia USD 2,500.
    Kwa kweli sisi kama wanafamilia wa mpira wa miguu hapa nchini lazima tutoe pongezi za dhati kwa SportPesa. Licha ya kudhamini klabu kadhaa za mpira wa miguu hapa nchini, michuano ya SportPesa Cup imekuwa ni chachu ya kuwajengea wachezaji wetu hali ya kujiamini na uzoefu wa mechi wa mechi za kimataifa kwa imekuwa ikishirikisha timu kutoka nje ya Tanzania. Kucheza mechi za ushindani nje ya nchi ni moja ya sababu ya kuendelea kufanya vizuri kwa timu yetu ya Taifa. Alisema Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa miguu Tanzania (TFF) Wilfred Kidao huku akisema kuwa TFF itaendelea kufanya kazi sambamba na SportPesa ili kuendelea kukuza soka hapa nchini.
    Wakati huo huo, Klabu ya Yanga kupitia kwa Kaimu Katibu Mkuu Omary Kaya imetoa pongezi kwa waandaji wa michuano ya SportPesa Cup ikisema kuwa ni kupima tosha kwa wachezaji wake. Michuano hii imekuwa ni moja ya njia ya klabu yetu kuweza kupata wachezaji tunaotaka kuwasajili lakini pia ni fursa kwa wachezaji wao kuweza kuonyesha vipaji vyao kwa wakala na ikiwezekana kuweza kupata timu za kuchezea nje ya nchi. Hata hivyo, Kaya alitoa wito kwa SportPesa na TFF kuweza kufanyia kazi kasoro ndogo ndogo ambazo zimekuwa zikijitokeza kwa ajili ya kuendelea kuboresha mashindano hayo.
    Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Singida United Festos Sanga alisema kuwa michuano hii imekuwa ikichochea na kuongeza hamasa ya wachezaji kitu ambacho kimeifanya timu hiyo kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu. Napenda kutoa pongezi kwa SportPesa kuweza kutangaza michuano hii mapema. 
    Hii itatoa nafasi kwa sisi kama klabu kuweza kujiandaa vyema kwa ajili ya kushiriki na nataka niseme tu kwa mwaka tutafanya vizuri na ikiwezekana kuwa bingwa na kuweka historia mpya.
    Klabu ya Mbao FC ambayo ndio inashiriki michuano hii kwa mara ya kwanza kupitia kwa Mwenyekiti wake Mr. Solly Zephania Njoshi imesema kuwa ni furaha kwa SportPesa kuweza kutambua uwezo wao na kuweza kuwashirikisha kwenye michuano ya SportPesa Cup kwa mara ya kwanza. Sisi kwetu ni furaha kubwa sana. 
    Kama mnavyojua tulipopanda daraja na kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza na msimu huo wa kwanza tukaweka historia, hivyo hivyo tutakapoweka historia kwenye michuano hii kwani sisi kila mechi tutachukulia kama fainali, alisema Zephania.
    Michuano ya awamu ya tatu ya SportPesa Cup 2019 itaanza kutimua vumbi mnamo Januari 22 mpaka na 27 2019 na itachezwa jijini Mwanza na Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza na kuwafikia mashabiki kwa urahisi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBAO FC WAINGIZWA MICHUANO YA SPORTPESA SUPER CUP 2019 BAADA YA KUIPIGA SIMBA SC 1-0 KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top