• HABARI MPYA

    Wednesday, October 03, 2018

    YANGA SC WAWAFUNGULIA MASHITAKA YA NGUMI SIMBA SC…MANARA AWAJIBU; “NA DANTE ALIPIGA KICHWA”

    Na Lulu Ringo, DAR ES SALAAM 
    KLABU ya Yanga SC imeandika barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kulalamika vitendo visivyo vya kiungwana walivyofanyiwa wachezaji wao na wachezaji wa mahasimu wao, Simba SC Jumapili katika pambano la Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Msemaji wa Yanga SC, Dissmas Ten amewaambia Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam kwamba wamelazimika kuyaripoti TFF baadhi ya matukio yaliyofanyika katika mchezo huo ili hatua zichukuliwe, akitolea mfano kitendo cha kiungo Mghana wa Simba SC, James Kotei kumpiga ngumi beki wao, Gardiel Michael na refa Jeonesiya Rukyaa wa Kagera hakuchukua hatua.

    Gardiel Michael alipigwa ngumi na James Koteli Jumapili Simba na Yanga zikitoka sare ya 0-0

    “Kwenye mchezo uliopita kuna matukio ambayo si ya kiungwana yalitokea uwanjani, sisi kama klabu tumeandika barua kwenda TFF na bodi ya Ligi kuomba mamlaka hizo kuchukua hatua stahiki kwa matukio yote yasiyo ya kiungwana yaliyotokea,” amesema Ten na kuongeza.
    “Huwezi kusema sana kulingana na mchezaji aliyefanya hayo matukio, mfano mchezaji wa kimataifa James Kotei ni mchezaji mzuri, hajawa na rekodi ya kufanya mambo ya kihuni uwanjani, hizi mechi zina mambo mengi, yawezekana alikutwa na mambo ambayo hata yeye hajui ni kitu gani kilimkumba kimsingi ilitosha yeye kuomba radhi hata kwa kutumia mitandao ya kijamii kama mchezaji muungwana” amesema.
    Lakini Msemaji wa Simba SC, Hajji Sunday Manara amemjibu Ten akisema kwamba hata wachezaji wa Yanga walifanya matukio yasiyo ya kiungwana kwenye mchezo huo akitolea mfano kitendo cha beki Andrew Vincent ‘Dante’ kumpiga kichwa Nahodha wao, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
    "Hatukuwa wajinga tulipoamua kukaa kimya, tumewasaidia wale waliokwenda kushitaki TFF na Bodi ya Ligi na hili pia walipeleke. Yule karusha ngumi na huyu kapiga kichwa,”amesema Manara na kuongeza; “Tukemee vitendo vyote vya kihuni Uwanjani siyo vya Simba tu,".
    Manara amesema kwamba mchezaji anaporusha kichwa kwa mwenzake kwa dhamira ovu,haijalishi kimemuathiri kwa kiasi – lakini anastahili kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na dhamira pekee.
    “Kama ilivyokuwa kwa Kotei, mliokwenda kumshitaki, sawa ni hivi, hatuungi mkono vitendo hivi na tunavikemea, ila tusiegemee upande mmoja, si Dante wala Kotei waliofanya sahihi, adhabu ikija ije kwa wote, wakiachiwa ni wote,”amesema Manara.
    Baada ya kushindwa kufungana katika dakika 90 za mchezo wa Jumapili, sasa mechi inaonekana kuhamia nje ya Uwanja kwa malumbano baina ya Wasemaji wa timu hizo juu ya matukio yaliyojitokeza siku hiyo. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAWAFUNGULIA MASHITAKA YA NGUMI SIMBA SC…MANARA AWAJIBU; “NA DANTE ALIPIGA KICHWA” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top