• HABARI MPYA

    Sunday, October 07, 2018

    YANGA SC INAHITAJI KOCHA WAKE WA KUWA KAZINI MUDA WOTE SI ZAHERA ANAYETUMIKIA ‘MABWANA WAWILI’

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    WAKATI Mbelgiji, Patrick Aussems aliiongoza Simba SC kupata ushindi wa 2-1 dhidi ya African Lyon jana, Yanga SC itamkosa kocha wake Mkuu, Mwinyi Zahera ikimenyana na Mbao FC kuanzia Saa 1:00 usiku wa leo Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara. 
    Zahera pamoja na kuwa kocha Mkuu wa Yanga SC, bado anaendelea kuwa Kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya kwao, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), maarufu The Leopard, yaani Chui – wakati Aussems ni kocha wa Simba tu, analala anaota na anashinda anawaza na kutumikia bwana mmoja tu.
    Na wakati huu wa mapumziko ya kupisha mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon, Zahera amekwenda kuungana na mkuu wake, Florent Ibenge kuiandaa timu yao kwa ajili ya mchezo wa Kundi G dhidi ya Zimbabwe Jumamosi ijayo mjini Kinshasa.

    Mwinyi Zahera (katikati) akiwa na Kocha Msaidizi, Mzambia, Noel Mwandila (kulia) na Mratibu, Hafidh Saleh (kushoto)

    Zahera aliwasili Yanga SC Mei mwaka huu kuchukua nafasi ya kocha Mzambia, George Lwandamina na baada tu ya kusaini mkataba wa miaka miwili akarejea kwao, Kinshasa kwa ajili ya kuiandaa The Leopard kwa mchezo wa kirafiki dhidi ya Nigeria mjini Port Harcourt Mei 28.
    Hakuna shaka kuhusu Zahera juu ya uwezo wake, kwani ni kocha mzoefu aliyezifundisha pia DC Motema Pembe ya kwao, DRC tangu Machi 1, mwaka 2015 hadi Machi 10, 2016, akitoka kuwa kaimu kocha wa AFC Tubize ya Ubelgiji kati ya Oktoba 7 na Oktoba 23, mwaka 2014 ambayo alijiunga nayo akitoka kuwa Kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya DRC kati ya Agosti 14 na 28, mwaka 2017 chini ya Ibenge.
    Alikuwa anafundisha AFC Tubize kwa mara ya pili, baada ya awali kuifundisha kama Kocha Mkuu kuanzia Julai 1 hadi Oktoba 20, mwaka 2010.
    Zahera Mwinyi alizaliwa Oktoba 19, mwaka 1962 kabla ya kuanza soka mwaka 1975 akiichezea klabu ya Bankin ya Goma, Kaskazini mwa jimbo la Kivu, DRC hadi mwaka 1980.
    Baadaye akaenda Kinshasa kucheza soka na kujiendeleza kielimu, akijiunga na Chuo cha Teknolojia (ISTA) huku akichezea klabu ya Sozacom hadi alipokutana na wakala wa wachezaji, Mbelgiji Karl Broken aliyemchukua na kumpeleka Ulaya kucheza soka ya kulipwa.
    Mwinyi Zahera alicheza kwa misimu miwili Antwerp FC ya Ubelgiji kabla ya kumaliza mkataba wake na kwenda Ufaransa alikochezea timu za Daraja la Pili, Amiens, Beauvais na Abbeville hadi akastaafu soka.
    Baada ya hapo akaanza kupata mafunzo ya ukocha, Zahera Mwinyi ambako alitunukiwa Diploma na leseni A ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA) kabla ya kuifundisha klabu ya SC Feignies ya Ufaransa kuanzia mwaka mwaka 2000 hadi 2010 kwa mafanikio makubwa kabla ya kwenda Ubelgiji kuifundisha Tubize na baadaye kutrejea nyumbani, DRC.
    Wasiwasi ni kwamba Zahera anataka kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja, zaidi kwa faida yake binafasi na kwa mtaji huo lazima kuna upande utaathirika – na muathirika hapo ni Yanga kwa sababu mashindano ya klabu yanaposimama ni yameisha au kupisha mechi za kimataifa.
    Hivyo ndivyo vipindi makocha wengine huvitumia kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza katika timu zao, ambayo katika Yanga yapo mengi mno na ndiyo maana kuficha udhaifu walicheza kwa kujihami dhidi ya Simba SC.
    Wiki hizi mbili ilikuwa fursa nzuri kwa Zahera kujumuisha wachezaji wa timu ya vijana katika mazoezi yake kuangalia wa kuongeza katika kikosi cha kwanza labda – lakini kubwa ni kufanyia kazi mapungufu yanayojitokeza.
    Lakini Zahera anabaki kuwa mtu wa kuiandaa tu timu kwa ajili ya mechi za Ligi na si kutengeneza timu kwa ujumla, hii maana yake itachukuwa muda kuona mabadiliko haswa ya kiuchezaji Yanga zaidi ya mbinu za ujanja ujanda kama hizo za ‘kupaki basi’.
    Na kwa mantiki hiyo Zahera ataendelea tu kuwatupia lawama wachezaji kwa kutocheza atakavyo, kwa kuwa hana muda wa kutosha wa kuwaelekeza na kuwapa maarifa mapya kutokana na kuwa mtumishi wa mabwana wawili.
    Zahera anaweza kuwa kocha mzuri sana, lakini kama hana muda wa kutosha wa kuitumikia Yanga mashabiki wa timu hiyo wasitarajie maajabu.
    Kuna makocha wengi sana, wazuri na wengine wa gharama nafuu kuliko Zahera – hivyo hakuna sababu Yanga kufanywa ‘ofisi ndogo’ wakati ina mahitaji makubwa.
    Yanga ni klabu kubwa na ina mahitaji makubwa, hivyo inahitaji kocha wa kuwa kazini muda wote apange programu za muda mfupi, wa kati na mrefu na si ‘kocha kibarua’. Ndiyo, inaonekana Zahera ni mwajiriwa wa DRC, huku Yanga anafanya kazi tu kipindi ambacho hana majukumu yake ya kawaida.
    Wapenzi wa Yanga wa siku hizo ni wabishi mno kama ilivyo wa Simba tu, hawapendi kusikia timu zao zinakosolewa kwa vyovyote – hawataki hata kujisumbua kupitia kilichoandikwa na kukifanyia kazi hata kama ni kwa maslahi ya klabu zao wenyewe.
    Sishangai wakatokea ‘wehu’ wa kuvurumisha matusi badala ya hoja za kupingana na hoja zilizoainishwa katika makala haya, ambayo msingi wake mkuu ni kutaka Yanga iwe na kocha wa kudumu na si ‘deiwaka’. 

    Patrick Aussems analala anaota, anashinda anawaza na kutumikia bwana mmoja tu, Simba SC

    Wengine wataleta hoja za eti Hemed Morocco ni kocha wa Singida United na Kocha Msaidizi wa timu ya taifa ya Tanzania ili kuhalalihsa Zahera naye kutumikia mabwana wawili, lakini wanasahahu kwamba mahitaji ya Yanga ni makubwa.
    Lakini, hadi hapa kuna mpenzi wa soka nchini hajaona tofauti ya Singida United iliyokuwa kocha wa kudumu msimu uliopita, Mholanzi Hans van der Pluijm na hii ya Morocco anayetumikia mabwana mawili? 
    Zahera lazima aamue kuchana kandarasi moja, ama ya Shirikisho la Soka la DRC, au ya Yanga – lakini kuendelea kutumikia mabwana wawili siyo sawa na hakuna ulazima huo kwa sababu kuna makocha wengine wengi bora hawana kazi. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC INAHITAJI KOCHA WAKE WA KUWA KAZINI MUDA WOTE SI ZAHERA ANAYETUMIKIA ‘MABWANA WAWILI’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top