• HABARI MPYA

    Saturday, October 13, 2018

    WATU 20 WANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA UCHUNGUZI ZAIDI JUU YA KUTEKWA KWA MO DEWJI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amesema kwamba watu 20 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi nchini hadi sasa kwa ajili ya uchunguzi juu ya kutekwa kwa Mfanyabiashara Bilionea, Mohammed ‘Mo’ Dewji juzi.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Lugoma amesema kwamba Jeshi la Polisi nchini linaendelea kumtafuta mfayabiashara huyo likiwa na imani kubwa ya kumpata akiwa salama.
    Waziri Lugola amelitaka jeshi la Polisi kuharakisha upelelezi wake ili lisiwashikilie washukiwa kwa zaidi ya saa 24.
    Aidha, Waziri Lugola amewataka wananchi kutoa taarifa zitakazoweza kulisaidia Jeshi la Polisi kupatikana kwa Mohammed Dewji.

    Watu 20 wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa uchunguzi juu ya kutekwa kwa Mfanyabiashara Mohammed ‘Mo’ Dewji 

    “Sababu za matukio ya kutekwa yanayotokea ni pamoja na kisiasa, kiuchumi, kimapenzi na njaa ili mtu apate fedha na sababu za kutekwa kwa Mohamed Dewji zitajulika hapo wahalifu watakapojulikana,” amesema Lugola. 
    Dewji mwenye umri wa miaka 43 alitekwa juzi asubuhi akiwa anaingia katika gym ya Collessium eneo la Masaki mjini Dar es Salaam kufanya mazoezi baada ya watu wasiojulikana kufyatua risasi hewani mfululizo wakati bilionea huyo anateremka kwenye gari yake kabla ya kumbeba na kumpakia kwenye gari lao na kutokomea naye kwa kasi.
    Mohammed, mtoto wa mfanyabiashara wa siku nyingi, Gulamabbas Dewji – ni rais wa makampuni MeTL Group yaliyoasisiwa na baba yake huyo ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Singida Mjini kwa tiketi ya CCM kati ya mwaka 2005 na 2015. 
    Februari mwaka huu ilielezwa utajiri wa Dewji unafikia dola za Kimarekani Bilioni 1.5 hivyo kushika nafasi ya 17 katika orodha ya matajiri wa Afrika na kuwa mfanyabiashara kijana tajiri zaidi.
    Kwa sasa, Mo Dewji yuko mbioni kuwa mmiliki wa klabu ya Simba kufuatia mkutano wa wanachama wa Desemba 3, mwaka jana kuazimia kumfanya bilionea huyo kuwa mwanahisa mkuu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
    Siku hiyo, Dewji alikubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye mwenyewe awali. 
    Ikumbukwe Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
    Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WATU 20 WANASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KWA UCHUNGUZI ZAIDI JUU YA KUTEKWA KWA MO DEWJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top