• HABARI MPYA

    Sunday, October 07, 2018

    VIONGOZI TFF WAACHE UBISHI, SIMBA NA YANGA ICHEZESHWE NA MAREFA WA KIGENI TU

    KLABU ya Yanga SC imeandika barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kulalamika vitendo visivyo vya kiungwana walivyofanyiwa wachezaji wao na wachezaji wa mahasimu wao, Simba SC Jumapili iliyopita, Septemba 30 katika pambano la Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Msemaji wa Yanga SC, Dissmas Ten aliwaambia Waandishi wa Habari mwanzoni mwa wiki hii mjini Dar es Salaam kwamba wamelazimika kuyaripoti TFF baadhi ya matukio yaliyofanyika katika mchezo huo ili hatua zichukuliwe, akitolea mfano kitendo cha kiungo Mghana wa Simba SC, James Kotei kumpiga ngumi beki wao, Gardiel Michael na refa Jeonesiya Rukyaa wa Kagera hakuchukua hatua.

    “Kwenye mchezo uliopita kuna matukio ambayo si ya kiungwana yalitokea uwanjani, sisi kama klabu tumeandika barua kwenda TFF na bodi ya Ligi kuomba mamlaka hizo kuchukua hatua stahiki kwa matukio yote yasiyo ya kiungwana yaliyotokea,” amesema Ten na kuongeza.
    “Huwezi kusema sana kulingana na mchezaji aliyefanya hayo matukio, mfano mchezaji wa kimataifa James Kotei ni mchezaji mzuri, hajawa na rekodi ya kufanya mambo ya kihuni uwanjani, hizi mechi zina mambo mengi, yawezekana alikutwa na mambo ambayo hata yeye hajui ni kitu gani kilimkumba kimsingi ilitosha yeye kuomba radhi hata kwa kutumia mitandao ya kijamii kama mchezaji muungwana” amesema.
    Lakini Msemaji wa Simba SC, Hajji Sunday Manara alimjibu Ten akisema kwamba hata wachezaji wa Yanga walifanya matukio yasiyo ya kiungwana kwenye mchezo huo akitolea mfano kitendo cha beki Andrew Vincent ‘Dante’ kumpiga kichwa Nahodha wao, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
    "Hatukuwa wajinga tulipoamua kukaa kimya, tumewasaidia wale waliokwenda kushitaki TFF na Bodi ya Ligi na hili pia walipeleke. Yule karusha ngumi na huyu kapiga kichwa,”amesema Manara na kuongeza; “Tukemee vitendo vyote vya kihuni Uwanjani siyo vya Simba tu,".
    Manara amesema kwamba mchezaji anaporusha kichwa kwa mwenzake kwa dhamira ovu, haijalishi kimemuathiri kwa kiasi – lakini anastahili kutolewa nje kwa kadi nyekundu kutokana na dhamira pekee.
    “Kama ilivyokuwa kwa Kotei, mliokwenda kumshitaki, sawa ni hivi, hatuungi mkono vitendo hivi na tunavikemea, ila tusiegemee upande mmoja, si Dante wala Kotei waliofanya sahihi, adhabu ikija ije kwa wote, wakiachiwa ni wote,”amesema Manara.
    Dakika 90 za mechi hiyo iliyochezeshwa na refa wa kike, Jeonisya Rukyaa ilimalizika kwa sare ya bila kufungana na kilichofuata ni malalamiko ya kimaamuzi.
    Wote, Ten na Manara walisema kweli juu ya matukio hayo ya kupiga kichwa na kupiga ngumi – bahati mbaya kuna matukio mengine ambayo hayajazungumzwa yalitokea na yalistahili adhabu za kadi nyekundu, lakini refa Jeonisya Jeonisya aliyekuwa akisaidiwa na Ferdinand Chacha wa Mwanza na Mohamed Mkono wa Dar es Salaam hakuyachukulia hatua.
    Jeonisya alikuwa radhi kuingia katikati ya wachezaji kuwaachanisha baada ya kushikana na kufanyiana mambo ambayo kikanuni yanastahili adhabu kuliko kutoa adhabu yenyewe.
    Kwake, hilo lilikuwa pambano la tatu la watani wa jadi wa soka ya Tanzania baada ya awali kuchezesha mechi mbili, Desemba 13, mwaka 2014 mechi ya Nani Mtani Jembe, Simba SC wakishinda 2-0, mabao ya Awadh Juma na Elias Maguri na ya pili Februari 20, mwaka 2016 Yanga SC wakishinda 2-0, mabao ya Donald Ngoma na Amissi Tambwe. 
    Lakini tathmini zinaonyesha bora mechi mbili za mwanzo aliziongoza vizuri kwa utafsiri wake wa sheria na zote alitoa kadi nyekundu, lakini Jumapili inaonekana alijiapiza kutotoa kadi hata iweje.
    Maana ukitazama matukio ya Kotei kumpiga ngumi Gardiel na Dante kumpiga kichwa Tshabalala yote aliyaona – hata lile la Pascal Wawa wa Simba kumpiga Heritier Makambo wa Yanga aliliona. Alisita kumuonyesha kadi ya pili ya njano Yondan kwa sababu alijua kifuatacho nyekundu. 
    Leo watu wanazungumza katika hali ya kawaida kwa sababu mechi iliisha 0-0, lakini kwa matukio yale yale timu ingefungwa mihemuko ingekuwa zaidi. Lakini, ni kosa kutochukua hatua sahihi kimaamuzi katika mchezo wa soka – hii inaamanisha umakini wa refa haukuwa wa kutosha.
    Tatizo la umakini mdogo kwa marefa limekwishaleta matatizo makubwa katika hizi za mechi za mahasimu wa jadi na kuhatarisha kabisa amani uwanjani.
    Maamuzi ya utata ya refa Martin Saanya yalisababisha vurugu Uwanja wa Taifa Jumamosi ya Oktoba 1, mwaka 2016 baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Tambwe alifunga bao hilo dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
    Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga. Na katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
    Kwa hali hiyo, mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani. Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
    Awali, Mpenzu alikataa bao safi la Simba lililofungwa na Ibrahim Ajib mapema kipindi cha kwanza akidai aliotea.
    Mwishowe, Saanya alifungiwa miaka miwili kwa pamoja na Msaidizi wake, namba moja, Samuel Mpenzu kwa kuvurunda na Kamati ya Masaa 72 ya Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikafuta Kadi nyekundu ya Mkude baada ya kubaini hakufanya kosa.
    Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi alinusurika katika tukio la hatari Machi 31, mwaka 2002 katika fainali ya Kombe la Tusker, Simba ikishinda 4-1.
    Siku hiyo refa Abdulkadir Omar ‘Msomali’ aliivuruga mechi na kuhatarisha amani uwanjani pia kwa madudu yake.
    Mechi hiyo ya fainali ambayo Alhaj Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa alikuwa mgeni rasi – chupuchupu  ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka Suleiman kufunga bao ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa. 
    Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za maji na mashabiki wa Yanga. Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza mchezo. 
    Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea kushuhudia mchezo huo. Baada ya hapo, alifungiwa na Chama cha Soka Tanzania, (FAT), sasa TFF kabla ya kujiuzulu uongozi wa klabu hiyo baadaye.
    Na ukitazama namna ambavyo marefa huwa ‘wanaharibu’ kwenye hizi mechi utagundua ni kwa sababu za kawaida sana ambazo jibu lake ni kuamua tu mechi hiyo ichezeshwe na marefa wa kigeni. 
    Watu bado wanakumbuka refa kutoka Uganda, Dennis Bate alivyochezesha vizuri fainali ya mwisho ya Kombe la Tusker mwaka 2009 kati ya Simba na Yanga – kuna kila sababu ya TFF kufanya maamuzi magumu kwa ustawi wa mechi hiyo iitwayo ya “Mahasimu", au "Watani wa Jadi”, Fahari pekee kubwa iliyobaki ya soka ya Tanzania. Jumapili njema. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VIONGOZI TFF WAACHE UBISHI, SIMBA NA YANGA ICHEZESHWE NA MAREFA WA KIGENI TU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top