• HABARI MPYA

  Tuesday, October 02, 2018

  ULIMWENGU WA KWANZA ANAYECHEZA NJE KURIPOTI KAMBINI TAIFA STARS MAANDALIZI MECHI NA CAPE VERDE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MSHAMBULIAJI wa El Hilal ya Sudan amekuwa mchezaji wa kwanza anayecheza nje kuripoti kwenye kikosi cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichoingia kambini jana kwenye hoteli ya Sea Scape iliyopo Kunduchi mjini Dar es Salaam kujiandaa na mechi mbili za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) dhidi ya Cape Verde.
  Taifa Stars watakuwa wageni wa Cape Verde katika mchezo wa Kundi L kufuzu AFCON Oktoba 12 mjini Praia kabla ya kurejea Dar es Salaa kwa mchezo wa marudiano na wapinzani wao hao Oktoba 16.
  Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo amesema kwamba wachezaji 13 walikuwa mazoezini hadi leo jioni Uwanja wa JMK Park, eneo la Gerezani mjini Dares Salaam.

  Thomas Ulimwengu wa nne kutoka kulia akiwa mazoezini Taifa Stars leo Uwanja wa JMK Park mjini Dar es Salaam

  Amewataja wachezaji hao mbali na Ulimwengu ni makipa Aishi Manula wa Simba SC, Beno Kakolanya wa Yanga SC na Mohamed Abdulrahman wa JKT Tanzania, mabeki; Shomari Kapombe wa Simba SC, Gardiel Michael, Kelvin Yondani  na Andrew Vincent wa Yanga SC, viungo Jonas Mkude wa Simba SC, Feisal Salum wa Yanga SC, Salum Kihimbwa wa Mtibwa Sugar na washambuliaji John Bocco wa Simba SC na Kelvin Sabato wa Mtibwa Sugar.  
  Wote hao walikuwa chini ya usimamizi wa Kocha Mkuu Emmanuel Amunike, anayesaidiwa na Hemed Suleiman ‘Morocco’ na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi, wakati Mtunza Vifaa ni Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya.
  Ambao hawajaripoti ni mabeki Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Salum Kimenya wa Tanzania Prisons, Paulo Ngalema, Ally Sonso wa Lipuli FC, Aggrey Morris, David Mwantika, Abdallah Kheri na Abdi Banda Baroka FC ya Afrika Kusini.
  Wengine ni viungo ni Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El –Jadida ya Morocco, Mudathir Yahya, Frank Domayo wa Azam FC na Farid Mussa wa CD Tenerife ya Hispania na washambuliaji Nahodha Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji, Yahya Zayd wa Azam, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana na Shaaban Iddi Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania.
  Tanzania inashika nafasi ya tatu katika Kundi L ikiwa na pointi mbili tu baada ya sare zote katika mechi zake mbili za mwanzo, 1-1 na Lesotho nyumbani mwaka jana na 0-0 na Uganda ugenini mapema mwezi huu.
  Uganda wanaendelea kuongoza Kundi hilo kwa pointi zao nne, wakifuatiwa na Lesotho mbili sawa na Tanzania na mabao mawili ya kufunga, wakati Cape Verde wanashika mkia kwa pointi yao moja. 
  Kihistoria Tanzania imecheza fainali moja tu za AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria, tena enzi hizo bado zinajulikana kama Fainali za kombe la Mataifa Huru ya Afrika.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ULIMWENGU WA KWANZA ANAYECHEZA NJE KURIPOTI KAMBINI TAIFA STARS MAANDALIZI MECHI NA CAPE VERDE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top