• HABARI MPYA

  Sunday, October 14, 2018

  TUMEVUNA TULICHOPANDA, TUELEKEZE NGUVU KWENYE MCHEZO WA MARUDIANO TULIPE KISASI

  TIMU ya soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars juzi imepata kipigo cha kushitua cha mabao 3-0 kutoka kwa wenyeji, Cape Verde katika mchezo wa Kundi L  kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Praia.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa Mali, Boubou Traore, Drissa Kamory Niare na Baba Yomboliba, mabao yaliyoizamisha Taifa Stars leo yalifungwa na mshambuliaji wa klabu ya Partizan ya Ligi Kuu ya Serbia, Ricardo Jorge Pires Gomes na beki wa MOL Vidi FC ya Hungary Ianique dos Santos Tavares maarufu kama Stopira.
  Kwa matokeo hayo, Cape Verde imefikisha pointi nne, sasa ikishika nafasi ya pili kwenye Kundi L, nyuma ya Uganda  yenye pointi saba, wakati Leshoto na Tanzania zinafuatia. 
  Huo utakuwa mchezo wa tatu wa Taifa Stars katika kundi bila ushindi, baada ya awali kutoa sare za 1-1 na Lesotho Dar es Salaam na 0-0 na Uganda mjini Kampala.
  Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike akiiongoza Taifa Stars kwa mara ya pili leo tangu aanze kazi Agosti alifanya mabadiliko ya mapema tu dakika ya 38 akimtoa beki wa kushoto, Gardiel Michael na kumuingiza beki wa kulia Shomari Kapombe.
  Na alifanya mabadiliko hayo baada ya ukuta wake Stars kuruhusu mabao mawili ndani ya dakika nane, yote yakifungwa na kijana mwenye umri wa miaka 26, Gomes aliyekuwa mwiba mchungu kwa ngome ya Stars.
  Gomes alifunga bao la kwanza dakika ya 16 baada ya kupokea pasi ya Garry Rodrigues kutoka upande wa kulia na kumlamba chenga beki wa Nkana FC ya Zambia, Hassan Kessy kabla ya kufumua shuti lililompita kipa namba moja wa Tanzania, Aishi Manula.
  Gomes akafunga bao la pili dakika ya 23 akimalizia pasi maridadi ya Jorge Semedo aliyemtoka kiungo Himid Mao upande wa kushoto wa Uwanja.
  Na baada ya mabao hayo mawili, Stars ikajaribu kubadili mfumo wa uchezaji kwa kuanza kushambulia, lakini bahati mbaya hawakuwa na uwezo wa kuipenya ngome ya ‘Papa wa Bluu’.
  Cape Verde wakapata pigo mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya mshambuliaji wao tegemeo, Gomes kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo nafasi yake ikichukuliwa na Nuno Rocha dakika ya 53.
  Lakini bado Cape Verde iliendelea kuwa mwiba na mara mbili ililitia musukosuko lango la Taifa Stars, lakini umaliziaji mbovu ukawanyima mabao zaidi.
  Taifa Stars ikapata uhai na kuanza kushambulia baada ya Amunike kuongeza idadi ya washambuliaji akimuingiza Nahodha wa Simba SC ya nyumbani kuchukua nafasi ya kiungo Mudathir Yahya.
  Na hiyo ikawagharimu kufungwa bao la tatu kwa shambulizi la kushitukiza, mfungaji beki wa kushoto  Ianique Tavares ‘Stopira’ dakika ya 85 aliyemalizia kwa kichwa kona ya Nuno Rocha. Kufika hapo, Taifa Stars wakawa wamekwishakubali matokeo na kucheza ili kumalizia mechi.
  Timu hizo zitarudiana mjini Dar es Salaam Jumanne na Taifa Stars itahitaji kushinda siyo tu kulipa kisasi, bali pia kufufua matumaini ya kufuzu AFCON ya mwakani nchini Cameroon.
  Baada ya kipigo cha juzi Watanzania wanaonekana kutumbukiwa nyongo na timu yao, wakiamini huo ndiyo mwisho wa ndoto za kwenda AFCON.
  Ikumbukwe Tanzania imecheza fainali moja tu za AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria, tena enzi hizo bado zinajulikana kama Fainali za kombe la Mataifa Huru ya Afrika (CAN).
  Kama nchi tulijiaminisha mno kupata matokeo mazuri Cape Verde baada ya kupitia rekodi ya wapinzani wetu katika mechi za awali – walikutana nasi wakiwa wanashika mkia katika kundi baada ya sare moja na Lesotho ugenini baada ya kufungwa nyumbani 1-0 na Uganda.
  Na kwa sababu sisi tulipata sare na Uganda mjini Kampala, tulijiona tuna ubora wa kwenda kuwafunga Cape Verde kwao, pasipo kutazama takwimu muhimu kama viwango vya FIFA au kuoanisha rekodi zetu na zao siku za karibuni.
  Cape Verde wamecheza fainali mbili mfululizo za AFCON mwaka 2013 na 2015 na kwa sasa wanashika nafasi ya 67 kwa ubora wa soka katika viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
  Katika mechi tatu zilizopita kabla ya kukutana nasi, Cape Verde hawakupoteza hata moja, wakishinda moja, 3-2 Juni 2 dhidi ya Algeria Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers na wakashinda kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0 na Andorra Juni 3, mwaka huu Uwanja wa Manispaa ya Jose Martins Vieira mjini Almada, zote za mechi za kirafiki.
  Lakini pia walitoa sare ya 0-0 ugenini na Lesotho Septemba 9, mwaka huu Uwanja wa Setsoto mjini Maseru, mechi ya Kundi L kufuzu AFCON kabla ya jana kutushughulikia sisi.
  Kwa upande wetu tunakumbuka katika mechi tatu zilizopita kabla ya kukutana na zahma ya jana, tumefungwa moja 4-1 na Algeria Machi 22, Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers, ikashinda 2-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Machi 27 nyumbani Dar es Salaam zote za kirafiki na baadaye sare ya 0-0 Uganda Septemba 8 mjini Kampala kufuzu AFCON 2019.
  Kwa rekodi hizi huwezi kuona sisi Tanzania ambao tunashika nafasi ya 140 kwenye renki za FIFA tulijidanganya nini hata tukaamua kuidharau Cape Verde na matokeo yake ndiyo kile kilichotokea jana.
  Nguvu na nidhamu tuliyoingia nayo kwenye mechi za Uganda mwezi uliopita vilitusaidia kupata pointi ugenini, kwa sababu mapema tu tuliwaaminisha wachezaji kwamba tunakwenda kwenye mechi ngumu.
  Lakini kwa kuwa tuliwaaminisha ushindi wachezaji wetu dhidi ya Cape Verde nao waliingia uwanjani wakiwa wamekwishashinda – waliwachukulia tofauti na walivyo wapinzani wao na matokeo yake ndiyo yale.
  Pamoja na yote, tunapaswa kusahau matokeo ya juzi na kuelekeza nguvu zetu katika mchezo ujao Jumanne kuhakikisha tu tunapata ushindi na kuamsha matumaini ya kufuzu AFCON.
  Tuamini wachezaji wetu wamejifunza kutokana na makosa yao juzi. Tuamini kocha Mkuu, Amunike ameona mapungufu na makosa yote. Tuamini viongozi wa timu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) nao kwa upande wao wameona walipokosea na wamejifunza pia.
  Nasi wananchi, kwa nafasiu zetu kama wapenzi wa timu tunapaswa kusahau yaliyopita na kuendelea kuisapoti timu yetu kuelekea mchezo wa marudiano keshokutwa ili tushinde na kufufua matumaini ya kwenda AFCON mwakani. 
  Hajafungwa Aishi Manula, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Aishi Manula, Hassan Kessy au Gardiel Michael, imefungwa Taifa Stars. Hajafungwa Amunike, wala Wallace Karia (Rais wa TFF), tumefungwa Watanzania wote. 
  Tuunganishe nguvu zetu kama taifa kuelekea mechi ya marudiano Jumanne. Huu si wakati wa kuanza kuandika maneno ya kuwaudhi wachezaji wetu kwenye mitandao ya kijamii. Tuwasamehe na kuendelea kuwaunga mkono, tukiendeleza na dua Mungu atusaidie na sisi tushinde nyumbani.
  Mungu ibariki Tanzania. Mungu ibariki Taifa Stars. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TUMEVUNA TULICHOPANDA, TUELEKEZE NGUVU KWENYE MCHEZO WA MARUDIANO TULIPE KISASI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top