• HABARI MPYA

  Friday, October 12, 2018

  TAIFA STARS WATOTA PRAIA, WAPIGWA MABAO MAWILI NA MTU MMOJA, WALALA 3-0 KWA CAPE VERDE

  Na Mwandishi Wetu, PRAIA
  NDOTO za Tanzania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zimeanza kuyeyuka baada ya leo kuchapwa mabao 3-0 na wenyeji, Cape Verde katika mchezo wa Kundi L uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Praia.
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa wa Mali, Boubou Traore, Drissa Kamory Niare na Baba Yomboliba, mabao yaliyoizamisha Taifa Stars leo yamefungwa na mshambuliaji wa klabu ya Partizan ya Ligi Kuu ya Serbia, Ricardo Jorge Pires Gomes na beki wa MOL Vidi FC ya Hungary Ianique dos Santos Tavares maarufu kama Stopira.
  Cape Verde inapanda kileleni kwa wastani mzuri wa mabao baada ya kufikisha pointi nne, sawa na Uganda ambao kesho watacheza mechi ya tatu na Leshoto yenye pointi mbili sawa na Tanzania. 

  Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta leo Uwanja wa Taifa mjini Praia

  Huo utakuwa mchezo wa tatu wa Taifa Stars katika kundi bila ushindi, baada ya awali kutoa sare za 1-1 na Lesotho Dar es Salaam na 0-0 na Uganda mjini Kampala.
  Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike akiiongoza Taifa Stars kwa mara ya pili leo tangu aanze kazi Agosti alifanya mabadiliko ya mapema tu dakika ya 38 akimtoa beki wa kushoto, Gardiel Michael na kumuingiza beki wa kulia Shomari Kapombe.
  Na alifanya mabadiliko hayo baada ya ukuta wake Stars kuruhusu mabao mawili ndani ya dakika nane, yote yakifungwa na kijana mwenye umri wa miaka 26, Gomes aliyekuwa mwiba mchungu kwa ngome ya Stars.
  Gomes alifunga bao la kwanza dakika ya 16 baada ya kupokea pasi ya Garry Rodrigues kutoka upande wa kulia na kumlamba chenga beki wa Nkana FC ya Zambia, Hassan Kessy kabla ya kufumua shuti lililompita kipa namba moja wa Tanzania, Aishi Manula.
  Gomes akafunga bao la pili dakika ya 23 akimalizia pasi maridadi ya Jorge Semedo aliyemtoka kiungo Himid Mao upande wa kushoto wa Uwanja.
  Na baada ta mabao hayo mawili, Stars ikajaribu kubadili mfumo wa uchezaji kwa kuanza kushambulia, lakini bahati mbaya hawakuwa na uwezo wa kuipenya ngome ya ‘Papa wa Bluu’.
  Cape Verde wakapata pigo mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya mshambuliaji wao tegemeo, Gomes kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo nafasi yake ikichukuliwa na Nuno Rocha dakika ya 53.
  Bado Cape Verde iliendelea kuwa mwiba na mara mbili ililitia musukosuko lango la Taifa Stars, lakini umaliziaji mbovu ukawanyima mabao zaidi.
  Taifa Stars ikapata uhai na kuanza kushambulia baada ya Amunike kuongeza idadi ya washambuliaji akimuingiza Nahodha wa Simba SC ya nyumbani kuchukua nafasi ya kiungo Mudathir Yahya.
  Na hiyo ikawagharimu kufungwa bao la tatu kwa shambulizi la kushitukiza, mfungaji beki wa kushoto  Ianique Tavares ‘Stopira’ dakika ya 85 aliyemalizia kwa kichwa kona ya Nuno Rocha. Kufika hapo, Taifa Stars wakawa wamekwishakubali matokeo na kucheza ili kumalizia mechi.
  Timu hizo zitarudiana mjini Dar es Salaam Jumanne na Taifa Stars itahitaji kushinda siyo tu kulipa kisasi, bali pia kufufua matumaini ya kufuzu AFCON ya mwakani nchini Cameroon.
  Kikosi cha Cape Verde kilikuwa; Thierry Graca, Elvis Manuel Macedo, Ianique Tavares ‘Stopira’, Carlos Rodrigues, Heldon Ramos/Luis Carlos Soares dk80, Garry Rodrigues, Jeffry Fortes, Admilson Barros, Ricardo Gomes/Nuno Rocha dk53, Jorge Semedo na Tiago Almeida
  Tanzania; Aishi Manula, Hassan Kessy, Gardiel Michael/Shomari Kapombe dk38, David Mwantika/Ally Sonso dk72, Abdi Banda, Aggrey Morris, Himid Mao, Mudathir Yahya/John Bocco dk78, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Simon Msuva.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: TAIFA STARS WATOTA PRAIA, WAPIGWA MABAO MAWILI NA MTU MMOJA, WALALA 3-0 KWA CAPE VERDE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top