• HABARI MPYA

    Wednesday, October 03, 2018

    STARS KWENDA NA KURUDI CAPE VERDE KWA DREAMLINER, WAZIRI MWAKYEMBE ATANGAZA NAFASI 200 NA ZAIDI ZA MASHABIKI

    Na Lulu Ringo, DAR ES SALAAM
    WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amesema ndege ya DreamLiner ndiyo itaipeleka timu ya taifa, Taifa Stars nchini Cape Verde kwa ajili ya mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2019 utakaofanyika Oktoba 12 mjini Praia.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Waziri Mwakyembe amesema kwamba ndege hiyo itakayobeba na mashabiki pia, itausubiri msafara huo na kurejea nao baada ya mechi hiyo kwa ajili ya mchezo wa marudiano baina ya timu hizo Oktoba 16 mjini Dar es Salaam.
    “Kitendo cha timu kushuka Cape Verde na Dreamliner, tena ndege ya nyumbani, tayari tumekwishawapiga goli mbili, hizo goli nyingine namuachia Amunike (Emmanuel) na benchi la ufundi waongezee,” amesema Waziri Mwakyembe.
    Ndege ya Dreamliner itakayoipeleka Taifa Stars nchini Cape Verde kwa ajili ya mchezo wa Kundi L kufuzu AFCON 2019

    Waziri huyo amesema kwamba kuna nafasi zaidi ya 200 za mashabiki kusafiri na timu kwa ajili ya mchezo huo, kwani ndege ya Dreamliner ina uwezo wa kuchukua watu 200 (262), wakati msafara mzima wa Taifa Stars utakuwa na watu 31.
    Waziri amesema kila shabiki atalazimika kiasi cha dola za Kimarekani 1,500 (zaidi ya Sh. Milioni 3.5) kwa safari ya kwenda na kurudi Cape Verde na kwamba wanaweza kukamilisha mpango huo kwa kufika ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zilizopo Uwanja wa Karume, Ilala mjini Dar es Salaam. 
    “Wachezaji na viongozi watakaokwenda Cape Verde hawatazidi 31, Dreamliner ina uwezo wa kuchukua watu zaidi ya 200, hivyo tunaomba mashabiki wajitahidi kununua tiketi tukaishabikie timu yetu ya taifa,” amesema Waziri Mwakyembe.
    Tayari wachezaji 22 wamekwisharipoti kambini Taifa Stars hoteli ya Sea Scape iliyopo Kunduchi mjini Dar es Salaam kujiandaa na mechi mbili na asubuhi ya leo wote wamefanya mazoezi Uwanja wa JMK Park, eneo la Gerezani mjini Dares Salaam.
    Hao ni makipa Aishi Manula (Simba SC), Beno Kakolanya (Yanga SC) na Mohamed Abdulrahman (JKT Tanzania), mabeki; Shomari Kapombe (Simba SC), Salum Kimenya (Tanzania Prisons), Gardiel Michael (Yanga SC), Paulo Ngalema (Lipuli FC), Ally Sonso (Lipuli FC), Aggrey Morris (Azam FC), David Mwantika (Azam FC), Abdallah Kheri (Azam FC), Kelvin Yondani (Yanga SC) na Andrew Vincent ‘Dante’(Yanga SC).
    Wengine ni viungo ni Mudathir Yahya ( Azam FC), Frank Domayo (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Feisal Salum (Yanga SC) na Salum Kihimbwa (Mtibwa Sugar) na washambuliaji; John Bocco (Simba SC), Yahya Zayd (Azam), Kelvin Sabato (Mtibwa Sugar) na Thomas Ulimwengu (El – Hilal/Sudan).
    Wote hao walikuwa chini ya usimamizi wa Kocha Mkuu Emmanuel Amunike, anayesaidiwa na Hemed Suleiman ‘Morocco’ na Mnigeria mwenzake, Emeka Amadi, wakati Mtunza Vifaa ni Ally Ruvu na Madaktari Richard Yomba na Gilbert Kigadya.
    Ambao hawajaripoti ni mabeki Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia na Abdi Banda Baroka FC ya Afrika Kusini, viungo Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El –Jadida ya Morocco na Farid Mussa wa CD Tenerife ya Hispania na washambuliaji Nahodha Mbwana Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana na Shaaban Iddi Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania.
    Tanzania inashika nafasi ya tatu katika Kundi L ikiwa na pointi mbili tu baada ya sare zote katika mechi zake mbili za mwanzo, 1-1 na Lesotho nyumbani mwaka jana na 0-0 na Uganda ugenini mapema mwezi huu.
    Uganda wanaendelea kuongoza Kundi hilo kwa pointi zao nne, wakifuatiwa na Lesotho mbili sawa na Tanzania na mabao mawili ya kufunga, wakati Cape Verde wanashika mkia kwa pointi yao moja. 
    Kihistoria Tanzania imecheza fainali moja tu za AFCON, mwaka 1980 nchini Nigeria, tena enzi hizo bado zinajulikana kama Fainali za kombe la Mataifa Huru ya Afrika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS KWENDA NA KURUDI CAPE VERDE KWA DREAMLINER, WAZIRI MWAKYEMBE ATANGAZA NAFASI 200 NA ZAIDI ZA MASHABIKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top