• HABARI MPYA

    Thursday, October 11, 2018

    SIMBA SC YAFUTA MAZOEZI KUMUOMBEA DUA MO DEWJI APATIKANE SALAMA BAADA YA KUTEKWA LEO ASUBUHI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    UONGOZI wa klabu ya Simba SC leo umefuta mazoezi kutokana na simanzi baada ya mfadhili wa klabu hiyo, mfanyabiashara Mohammed ‘Mo’ Dewji kutekwa mapema leo asubuhi na watu wasiojulikana.
    Dewji alitekwa mapema leo asubuhi akiwa anaingia katika gym ya Collessium eneo la Masaki mjini Dar es Salaam kufanya mazoezi na tangu hapo Jeshi la Polisi linaendesha msako mkalio wa kumtafuta mfanyabiashara huyo.
    Msemaji wa klabu ya Simba SC, Hajji Sunday Manara amesema kwamba kwa mashauriano na Benchi la Ufundi chini ya kocha Mkuu, Mbelgiji Patrick J. Aussems klabu imefuta mazoezi kutokana na simanzi iliyopo.
    “Benchi la Ufundi chini ya Kocha Mkuu, Patrick Aussems limeamua kuahirisha mazoezi ya timu leo ili kutoa fursa kwa Wachezaji na Benchi la Ufundi kushiriki ipasavyo kwenye Dua na Sala kwa ajili ya kiongozi wetu,” amesema Manara.
    Mohammed Dewji ametekwa leo asubuhi akiwa anaingia katika gym ya hoteli yab Collessium, Oysterbay mjini Dar es Salaam kufanya mazoezi 

    Msemaji huyo amesema kwamba wanawaomba Watanzania na wanoitakia mema nchi yetu waendelee kumuombea uhai na uzima Mo Dewji, huku msako mkali ukiendeshwa na Jeshi la Polisi aweze kupatikana.
    Jioni hii, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema kwamba oparesheni kali bado inaendelea, lakini Mo Dewji hajapatikana.
    Mo Dewji mwenye umri wa miaka 43 alitekwa asubuhi ya leo akiwa anaingia kwenye gym hiyo kama ilivyo ada yake kila siku asubuhi kwa ajili ya mazoezi.
    Watu wasiojulikana walifyatua bunduki hewani mfululizo wakati Dewji anateremka kwenye gari yake kabla ya kumbeba na kumpakia kwenye gari lao na kutokomea naye kwa kasi.
    Mapema baada ya tukio, Kamanda Mambosasa alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watu watatu juu ya sakata hilo, lakini akasikitika kwamba kamera za CCTV za hoteli ya Collessium hazioneshi vizuri sehemu ambayo watekaji waliingilia.
    Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema kwamba ofisi yake na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wanashirikiana bega kwa bega na Jeshi la Polisi kuhakikisha mfanyabiashara huyo anapatikana.
    “Mpaka sasa Jeshi la polisi limekamata watu watatu waliohusika katika utekaji wa bilionea Mohamed 'Mo' Dewji. Mo tutampata na tutampata akiwa salama,”amesema Mo Dewji.
    Mohammed, mtoto wa mfanyabiashara wa siku nyingi, Gulamabbas Dewji – ni rais wa makampuni MeTL Group yaliyoasisiwa na baba yake huyo.
    Pamoja na biashara, Dewji amewahi kuwa Mbunge wa Singida Mjini kwa tiketi ya CCM kati ya mwaka 2005 na 2015. 
    Februari mwaka huu ilielezwa utajiri wa Dewji unafikia dola za Kimarekani Bilioni 1.5 hivyo kushika nafasi ya 17 katika orodha ya matajiri wa Afrika na kuwa mfanyabiashara kijana tajiri zaidi.
    Kwa sasa, Mo Dewji yuko mbioni kuwa mmiliki wa klabu ya Simba kufuatia mkutano wa wanachama wa Desemba 3, mwaka jana kuazimia kumfanya bilionea huyo kuwa mwanahisa mkuu katika mfumo mpya wa uendeshwaji.
    Siku hiyo, Dewji alikubali kununua asilimia 49 za hisa za klabu ya Simba SC kulingana na maelekezo ya Serikali badala ya asilimia 51 alizotaka yeye mwenyewe awali. 
    Ikumbukwe Mo pekee aliweka dau la Sh Bilioni 20 kuomba asilimia 50 ya hisa, baada ya klabu kutangaza kuuza asilimia 50 ya hisa zake kwa Sh. Bilioni 20 miezi miwili iliyopita, ingawa baadaye Serikali ikaagiza klabu hiyo isiuze zaidi ya asilimia 49 kwa mtu mmoja.
    Wanachama 1320 walihudhuria mkutano huo wa Desemba 3, mwaka jana kutoka Dar es Salaam na mikoa jirani na kwa furaha ya ushindi huo, Mo Dewji alitoa ahadi 10 za kuleta mabadiliko makubwa, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa mazoezi wa nyasi za asili na nyasi bandia pamoja na hosteli ya kisasa ya wachezaji. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAFUTA MAZOEZI KUMUOMBEA DUA MO DEWJI APATIKANE SALAMA BAADA YA KUTEKWA LEO ASUBUHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top