• HABARI MPYA

    Wednesday, October 10, 2018

    SERIKALI YAWATAKA WATANZANIA KUUENZI UTAMADUNI KWA SABABU NI SEHEMU YA UTALII

    Na Anitha Jonas, ARUSHA (WHUSM)
    SERIKALI imewataka watanzania kudumisha  na kurithisha amali za urithi wa asili wa utamaduni wa kitanzania kwa vijana na watoto kwa manufaa ya kizazi kijacho.
    Kauli hiyo imetolewa leo jijini Arusha na Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Susan Mlawi alipokuwa akifungua Tamasha la Urithi Festival kwa niaba ya Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Utamaduni Dk. Harrison Mwakyembe katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
    Akiendelea kuzungumza katika  sherehe hizo za ufunguzi wa Tamasha hilo Mlawi asisitiza kuwa uwepo wa tamasha hilo utatoa fursa mbalimbali kwa watanzania wa kunadi,kuonesha na kutangaza rasilimali za  utalii wa utamaduni  ndani na nje ya nchi.

    Wacheza ngoma jamii ya Wasonjo kutoka Ngorongoro wakicheza ngoma ya asili wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Urithi Festival leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha 

    Katibu  Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Susan Mlawi  akitizama  maziwa yanavyohifadhiwa kwenye kibuyu na mama wa Kimaasai, Neema Mollel wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Urithi Festival leo Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha

    “Uanuai wa Maendeleo ya sekta ya utalii wa kiutamaduni ili uishi na usiwe katika hatari ya kupotea unahitajika kutambua na kuthamini urithi wa Jadi kama Mila, Desturi, Lugha, Maadili na Imani hivyo uhifadhi, utafiti na utasaidia kunadi kutaendeleza rasilimali za asili za taifa,”alisema Mlawi.
    Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Urithi Festival Taifa Profesa Audax Mabula alieleza kuwa wazo la kuanzishwa kwa tamasha hilo lilitokea Wizara ya Maliasili na Utalii lengo likiwa ni kutangaza utalii wa kiutamaduni kwani Tanzania imebarikiwa kuwa na vivutio vingi vya kiutamaduni ambavyo ni hazina kuwa kwa Taifa.
    “Nchi yetu imebarikiwa kwa kuwa na vivutio vingi vya kiutamaduni kama michoro ya mapangoni inayopatika kama Kondoa,makundi manne ya lugha za afrika yanayopatikana mkoa wa Manyara na jirani,ngoma za asili kutoka makabila mbalimbali nchini pamoja na vyakula vya asili,”alisema Profesa Mabula.
    Aidha, nae Mkurugenzi Mkuu  Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyapori Tanzania Dk. James Wakibala  alitoa salamu za Waziri wa Maliasili Utamaduni Sanaa na Michezo kwa wadau wa Mkoa wa Arusha na viongozi wake waliyoshiriki tamasha hilo kwa kuwapongeza katika kushiriki tamasha hilo ambalo kwa namna moja litasaidia kuendeleza utalii katika sekta ya Utamaduni.
    Hata hivyo Katibu Mkuu huyo katika hitimisho la hotuba yake aliiomba Wizara hiyo ya Maliasili na Utalii kushirikiana na Wizara yake katika maandalizi ya tamasha hilo kwa mwakani kwani wote wanadhamana ya kukuza  na kutangaza utalii wa Kiutamaduni.
    Halikadhali hitimisho la Tamasha hilo kwa mwaka huu linatarajiwa kufanyika Oktoba 13, mkoani hapo na Waziri Mkuu wa Tanzania Mheshimiwa Kassim Majaliwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SERIKALI YAWATAKA WATANZANIA KUUENZI UTAMADUNI KWA SABABU NI SEHEMU YA UTALII Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top